Uchumi wa China waporomoka kwa asilimia 6.8
17 Aprili 2020Takwimu rasmi za serikali ya China zimeonyesha kuwa pato la taifa nchini humo limeshuka kwa asilimia 6.8 katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2020, ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho kwa mwaka 2019. Uchumi wa China umedorora kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Mapinduzi ya Kitamaduni mwaka 1976.
Anguko hilo la uchumi la kihistoria, ni la kwanza tangu China ilipoanza kuchapisha takwimu za pato la ndani kila baada ya miezi minne mwaka 1992, na linatokana na nchi hiyo kufunga viwanda na maduka makubwa pamoja na kusimamisha huduma ya usafiri kutokana na mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 ulioanzia China mwaka uliopita.
Hayo yanajiri wakati ambapo China imerekebisha takwimu zake za idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi vya corona kwa asilimia 50. Mji wa Wuhan ambako virusi hivyo vilianzia, umetangaza kwamba watu 1,290 zaidi walikufa kutokana na virusi vya corona, mbali na idadi iliyotangazwa awali ya vifo 2,579.
Marekani yatangaza kufanya uchunguzi
Taarifa hizo zimetangazwa Ijumaa, siku moja baada ya Marekani kusema itafanya uchunguzi kubaini kama China ilificha ukweli kuhusu mripuko wa virusi vya corona na hivyo kuifanya idadi jumla ya vifo kwenye mji huo kuwa 3,869. Hali kadhalika idadi jumla ya vifo vilivyotokea China sasa ni 4,632.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesema hakukuwa na aina yoyote ya kuficha taarifa za idadi ya vifo vya virusi vya corona kwenye mji wa Wuhan. Maafisa wa China wanasema sababu ya vifo hivyo kutojulikana ni kutokana na kutoripotiwa au idadi kupotoshwa.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza mipango ya kuanza kulegeza masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Ikulu ya Marekani imesema chini ya mipango hiyo iliyopewa jina ''Kuifungua Tena Marekani'', magavana wa majimbo wanaweza kuondoa masharti kwa awamu tatu. Rais Trump amesema hali ya kawaida itarejea hivi karibuni.
''Mwongozo wetu umetolewa kwa awamu tatu katika kurejesha maisha yetu ya kiuchumi. Hatufungui yote kwa wakati mmoja, lakini hatua kwa hatua huku tukiwa makini na baadhi ya majimbo yatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo mapema kuliko mengine,'' alifafanua Trump.
Mipango hiyo ni pamoja uwezakano wa kufunguliwa kwa makanisa na maeneo ya michezo kwa kuzingatia taratibu madhubuti za watu kutotengamana na watu wanaruhusiwa kutembea wakiwa katika kundi la watu 10. Takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 32,900 wamekufa kwa virusi vya corona nchini Marekani na takriban watu 630,000 wameambukizwa.
Aidha, Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn amesema wamefanikiwa kudhibiti maambukizi ya COVID-19. Akizungumza Ijumaa na waandishi habari mjini Berlin, Jens amesema ongezeko la visa vipya sio la kutisha. Takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Robert Koch zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaoambukizwa imepungua kwa 0.7 kutoka 1 katika siku chache zilizopita.
Ama kwa upande mwingine, Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro amemfukuza kazi Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Luiz Henrique Mandetta kutokana na mfululizo wa matukio ya kutokubaliana kuhusu namna ya kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.
(AP, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2yrxaTZ)