Uchumi wa Ujerumani waja juu, wa Ufaransa waporomoka
14 Agosti 2012Taifa lenye uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya, Ujerumani, limepanda juu kwa asilimia 0.3 ndani ya miezi mitatu iliyopita, likiuka hata matazamio ya wafuatiliaji wa masuala ya uchumi. Hata hivyo, bado inaaminika itakuwa shida kuepuka mvutano wa kiuchumi, ikiwa hatua kali na madhubuti hazikuchukuliwa kupambana na mzozo wa madeni kwenye eneo zima la sarafu ya euro.
Takwimu za karibuni kabisa za robo ya tatu ya mwaka zimeonesha kushuka kwa uzalishaji wa viwandani nchini Ujerumani na uingizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi. Jörg Krämer wa Benki ya Biashara ya Ujerumani, ameliambia Shirika la Habari la Reuters, kwamba licha ya ukuwaji wa uchumi kuwa mzuri safari hii, hiyo huenda ikawa sehemu pekee ya habari njema.
"Uchumi wa Ujerumani unaweza kushuka katika majira haya ya kiangazi. Kimsingi uko kwenye hali nzuri kwa sasa, lakini hauwezi kujitenga kutoka mgogoro wa kifedha katika kanda ya euro, ikijumlishwa pia na ukweli kwamba uchumi wa dunia nao umeshuka." Amesema Kräamer.
Ufaransa yaporomoka
Kwa upande wa Ufaransa, hii ni robo ya tatu mfululizo kujikuta ikiwa na ukuwaji sufuri. Tayari Benki Kuu ya nchi hiyo imeshasema kuwa inatarajia kushuka tena kwa kiwango cha kati kwa uchumi wa Ufaransa ndani ya robo ya tatu.
Kwa ujumla, uchumi katika kanda nzima ya euro unatazamiwa kushuka kwa asilimia 0.2 katika robo ya pili, baada ya kuwa ulisimama kwenye robo ya kwanza. Wataalamu wa uchumi wanasema hali mbaya zaidi inaweza kujitokeza, kwani Ujerumani peke yake haiwezi kuendelea kulifanya eneo zima la sarafu ya euro kuwa salama.
Mmoja wa wataalamu hao, Aline Schuiling wa ABN AMRO, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, licha ya ukuwaji wa uchumi wa Ujerumani, wanatarajia ukuwaji wa asilimia sufuri katika pato jumla la kanda ya euro kushuka hadi asilimia 0.4 katika robo ya pili, kutokana na hatua kali za kubana matumizi zinazoyafanya mataifa mengi zaidi kutumbukia kwenye mzozo wa madeni.
Mataifa ya euro kwenye wasiwasi
Mataifa ya kanda ya euro yaliyo kwenye ukingo wa kutumbukia kwenye mzozo wa madeni, yapo kwenye hatari zaidi sasa kuliko wakati mwengine huko nyuma. Hali ya uchumi kwenye mataifa hayo inaripotiwa kuzidi kutikisika huku mapato yatokanayo na kodi yakipungua na hivyo kuzifanya jitihada za kupunguza nakisi kuwa ngumu zaidi kufanikiwa.
Takwimu zilizochapishwa jana zilionesha kuwa hatua za kukata deni zilichangia kwa asilimia 6.2 kuutikisa uchumi wa Ugiriki katika robo ya pili, huku wataalamu wa uchumi wakisema hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu. Kwa upande wa Italia, uchumi wake ulinywea kwa asilimia 0.7, huku pato jumla katika uchumi wa Finland likianguka kwa asilimia 0.7 pia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman