1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi: Polisi wa mji alikouliwa Floyd ni wabaguzi

28 Aprili 2022

Uchunguzi uliofanywa jimboni Minnesota nchini Marekani umebaini kwamba maafisa wa polisi katika mji wa Minneapolis wana chembe chembe za "ubaguzi wa rangi".

Syrien Künstler Mural Aziz al Asmar
Picha: Izzeddin Idilbi/AA/picture alliance

Uchunguzi huo ulianzishwa kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd kilichotokea Mei mwaka 2020 huko Minneapolis.

Ripoti pana ya uchunguzi huo imebaini kuwa idara ya polisi ya mji huo imekuwa ikifanya vitendo vya "ubaguzi wa rangi" dhidi ya watu weusi kwa miongo kadhaa.

Uchunguzi huo uliofanywa na idara ya Haki za Binadamu ya jimbo la Minnesota imefichua tofauti kubwa jinsi maafisa wa polisi walivyokuwa wakitekeleza majukumu yao mbele ya watu wa rangi tofauti.

Kulikuwa na tofauti kubwa pindi polisi inapowasimamisha, kuwapekua, kuwakamata au kuwazungumzia watu wasio wazungu ikilinganishwa na walio weupe.

Mkuu wa uchunguzi asema mwenendo wa ubaguzi ni hatari 

Picha: Kerem Yucel/AFP/Getty Images

Ripoti imeonesha kuwa polisi ya mji huo ilifanya kuwa ni tabia ya kawaida kwa maafisa wake kuwatenga watu kwa makundi ya rangi zao wakati wa utekelezaji wao wa majukumu ya usimamizi wa sheria.

"Kusimamia utiifu wa sheria kwa kutizama rangi ya mtu ni kinyume cha sheria na inamdhuru kila mtu hususani jamii ya watu wasio weupe - na wakati mwingine imegharimu maisha ya baadhi yao" amesema kamishna wa Haki za Binadamu Rebecca Lucero katika taarifa aliyoitoa.

Ripoti imebaini aina hiyo ya usimamizi wa sheria ilikuwa ni sehemu ya "utamaduni wa idara ya polisi" inayosisitiza matumizi ya mbinu za zisizokubalika katika utekelezaji wa majukumu.

Mathalani polisi wa mji wa Minneapolisi walitumia mitandao ya kijamii kuwafuatilia watu weusi au taasisi ambazo hazina rikodi ya uhalifu lakini haikutumia mbinu hizo kwa makundi ya wazungu wabuguzi au wenye misimamo mikali.

Kadhalika maafisa wa polisi wamebainika walikuwa wakitumia "lugha ya kibaguzi kwa rangi na jinsia na lugha ya matusi".

Miaka miwili tangu kifo cha Floyd na lawama ya polisi wa Marekani 

Matokeo ya uchunguzi huo yametolewa miaka miwili tangu mauaji ya George Floyd yaliyofanywa na maafisa wa polisi kuzusha maandamano makubwa nchini Marekani na duniani kupinga ukatili wa polisi.

Picha: Brian Lawless/PA Wire/dpa/picture alliance

Mamlaka za jimbo la Minnesota uliko mji wa Minneapolis walianzisha uchunguzi wa haraka kufuatia miito ya nchi nzima iliyotaka idara za polisi zifutwe au kupunguziwa bajeti.

Wachunguzi walikusanya mikanda ya video yenye urefu wa saa kadhaa, kupitia ripoti za polisi na kufanya mahojiano na maelfu ya watu kabla ya kufikia hitimisho katika ripoti hiyo ya wiki hii.

Takwimu zao zimefichua kwa mwaka 2020  kati ya watu 14 waliouliwa na polisi wa Minneapolis, 13 hawakuwa wazungu ikiwemo George Floyd.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW