Uchunguzi ufanywe dhidi ya mauaji ya watoto Tanzania, THDRC
30 Januari 2019Tawi la Kanda ya Ziwa la mtandao wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania, THDRC limeitaka polisi nchini humo kufanya kila njia kuwabaini wote waliohusika katika mauaji ya watoto kumi mkoani Njombe. Sababu kubwa ya mauaji hayo inatajwa kuwa imani za kishirikina.
Wito huo umetolewa kwa pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania leo jijini Mwanza wakati wakizungumza na waandishi wa habari. Rebeca Mafipa ambaye ni Mratibu wa SHIRIKA la sauti ya wanawake anasema inahitajika nguvu ya pamoja kutoka kwa vyombo vya Usalama na Jamii ili kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za Binadamu.
Mauaji hayo ya watoto yameibua hofu kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Njombe, na hii leo, Serikali kupitia waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola, imetangaza mjini Dodoma kuwa itachukuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika. Hata hivyo bado wanaharakati wa haki za binadamu wanaona kumekuwa na udhaifu katika kuyadhibiti matukio ya ukiukwaji wa haki za Binadamu nchini Tanzania. Edwini Soko ni mwenyekiti wa asasi inayopinga uhalifu na dawa za kulevya nchini Tanzania.
Imani za kishirikina zimetajwa zimeelezwa kuwa sababu ya mauaji hayo ya watoto, hali ambayo imelalamikiwa na wadau wa haki za binadamu, wakisema haishughulikiwi vya kutosha na vyombo vya habari nchini Tanzania hususani katika kuyakabili matukio haya kabla kabla hayajatokea.
Matukio ya mauaji ya watoto mkoani Njombe mbali na kuibua simanzi kubwa kwa wafiwa pamoja na wanajamii wote,yanatokea katika kipindi ambacho kada ya wazee nchini imekuwa na kilio cha muda mrefu juu ya maisha yao baada ya kuwa wakiwindwa, huku jamii ya watu wenye albinism nayo ikiwa na kilio hicho hicho.
Mwandishi: Dotto Bulendu/DW-Mwanza
Mhariri: Gakuba, Daniel