1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa maabara waanzishwa Tanzania

4 Mei 2020

Serikali ya Tanzania imeanzisha uchunguzi katika maabara ya taifa inayotumika kupima sampuli za homa ya Covid-19, ikiwa ni siku moja baada ya rais wa taifa hilo, John Magufuli kutilia shaka mwenendo wa vipimo vyake.

Coronavirus in U.S. Navy
Picha: picture-alliance/Zuma/Planetpix/J. Berlier

Jopo la wataalamu tayari limeundwa kwa ajili ya kuendesha uchunguzi huo uliopangwa kukamilika kwa muda wa siku kumi kutoka sasa. Taarifa ya wizara ya afya inasema uchunguzi huo unafanywa na magwiji wa masuala ya sayansi kutoka vyuo mbalimbali nchini pamoja na madaktari.

Mbali ya kuanzishwa kwa uchunguzi huo, pia waziri wa afya ameagiza kusimamishwa kazi kwa watendaji wakuu wa maabara hiyo ya taifa ikiwamo mkurugenzi wake mkuu, hadi pale ripoti ya uchunguzi huo itakapotolewa.

Hayo yanakuja wakati Rais John Magufuli akimwachisha kazi mkurugenzi mkuu wa bohari ya taifa na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa mkuu wa hospitali ya jeshi Lugalo.

Wakati Tanzania ikianzisha uchunguzi huo kuhusu mwenendo wa maabara ya taifa, baaadhi ya mataifa duniani yamekuwa yakiripoti kuhusu kiwango duni kinachoonyeshwa na mashine zake zinazotumika kupima maambukizi ya virusi vya corona.

Kauli ya Rais Magufuli yaendelea kuzua gumzo ndani na nje ya Tanzania

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli Picha: DW/S. Khamis

Hatua ya Tanzania kuanzisha uchunguzi huo inakuja siku moja tu baada ya Rais Magufuli kutilia shaka mwenendo wa maabara hiyo pamoja na vifaa vinavyotumika kutambua watu walioambukiwa homa ya covid-19.

Rais Magufuli alisema sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wanyama kama mbuzi, kondoo, kware na oili zikibainika kuwa zimekumbwa na maambukizi ya ugonjwa huo unaoendelea kusumbua vichwa vya wengi duniani.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imeendelea kuzusha mjadala mkubwa katika makundi mbalimbali ya watu wanaotumia kauli hiyo kwa mitazamo tofauti. Akizungumza leo, jijini Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Pau Makonda amewataka wananchi kutoitafsiri vibaya kauli hiyo.

Ama serikali imetuliza hali ya wasiwasi iliyokuwa imetanda kwa wananchi wengi hasa wanaopoteza jamaa zao kwa janga hilo la corona ambao walikuwa wakishuhudiwa ndugu zao hao wakizikwa nyakati za usiku tena katika hali ya taharuki.

Serikali imesema hakuna haja ya kuwazika watu wanaofariki kwa corona wakati wa usiku na imewataka watendaji wake kufanya majadiliano na wahusika wa familia kabla ya kuchukua hatua ya kufanya maziko.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW