Uchunguzi wa maiti za maafa ya msitu wa Shakahola waanza
27 Aprili 2023Waziri wa Usalama wa taifa Kithure Kindiki amepiga marufuku kuingia kwenye shamba la Chakama la ekari 800 uliko msitu wa Shakahola huko Kilifi.Kwa mtazamo wake, eneo hilo ni la uhalifu.Kadhalika wizara ya usalama wa taifa imeandaa kituo maalum cha habari na maelezo kwenye lango la shamba la Chakama kuuwezesha umma kusaka jamaa zao na pia kupata usaidizi.Eneo la Chakama liko nje kidogo ya mji wa Malindi.Amina Mnyazi ni mbunge wa Malindi na huu ndio mtazamo wake.
Soma pia: Idadi ya watu waliokufa kwa kukataa kula kwa imani ya kwenda kwa Mungu yaongezeka hadi watu 98
Waziri Kindiki pia ameweka bayana kuwa wahalifu wanaojificha kwenye dini watachukuliwa hatua iwapo watakiuka sheria,dini na uhuru wa kuabudu kwa misingi ya katiba.Kindiki ameyasema hayo alipokizuru kijiji cha Shakahola alikofika kwenye msitu wa maafa.Hata hivyo mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Kilifi Getrude Mbeyu anamshinikiza waziri Kindiki kusogea kando kwani maafa hayo yametokea wakati wa utawala wake.
Marufuku ya kuingia kwenye Shamba la Chakama kutokea macheo hadi machweo tayari imetangazwa kwa siku 30 zijazo.Mbunge wa Magarini Harrison Garama Kombe anaisisitizia serikali kuwa mchungaji Mackenzie hapaswi kuruhusiwa kurejea Shakahola.
Yote hayo yakiendelea,mchungaji mwengine, Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer lililoko Mavueni kaunti ya Kilifi amekamatwa na polisi kwa madai ya mauaji kutokea kwenye kituo chake cha maombi ambacho sasa kimefungwa.
Waumini waliopatikana kwenye kanisa hii leo wanatakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi, amebainisha Waziri wa Usalama wa taifa Kithure Kindiki.TM,DW, Nairobi.