Udhalilishaji kingono umeenea Congo
19 Juni 2017Maelfu ya wasichana wadogo wamekamatwa ama kuingizwa katika majeshi ya wanamgambo kadhaa mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, ambako mara nyingi wanatumika kingono , kundi la kutetea haki za watoto la Child Soldiers International limesema leo.
Mashariki mwa Congo kuna mamia kwa maelfu ya wanajeshi watoto na wasichana ambao wanahusiana na makundi hayo yenye silaha, amesema Sandra Olsson kutoka kundi hilo la Child Soldiers International.
Wasichana wenye umri kutoka miaka tisa hadi 16 wanafanya kazi mbali mbali kwa ajili ya wanamgambo, ikiwa ni pamoja na kupika, ukusanya kuni, kubeba mali zilizoporwa, wakitumika pia kama watumwa wa kingono na hata kushiriki katika mapigano kama wanajeshi ama wapelelezi, Olsson ameliambia shirika la habari la dpa.
Kundi la Child Soldiers International pamoja na washirika wake wa Congo wamewahoji wasichana 150 kwa ajili ya ripoti itakayochapishwa leo.