UDONDOZI WA MAGAZETINI
17 Januari 2005Kuhusu hukumu katika kesi ya kuteswa wafungwa wa Kiiraq, gazeti la NÜRENBERGER NACHRICHTEN linaandika:
"Kule kudhihirishwa hadharani hukumu za wanajeshi wachache wenye hatia, hakusaidii kamwe kuwababaisha wenye akili zao wanaojua kwamba tangu lifanyike shambulio la Septemba 11, 2001 nchini Marekani, lile wimbi lililofuatilia la jazba na hamasa, na kule kwa Rais kutangaza vita dhidi ya ugaidi, kumeunda hali inayovumilia matumizi ya kila aina ya silaha. Ikiwa katika kambi la wanajeshi wa Kimarekani huko Guantanamo, Cuba, ikiwa ni katika vifungo vyake vya kijeshi huko Afghanistan au katika jela ya Abu Ghuraib huko Iraq, kote huko umejidhihirisha mfumo wenye kukiuka misingi ya usalama ya Kimarekani na ya Kimataifa."
Kwa mujibu wa gazeti la SAARBRÜCKER ZEITUNG: "Graner hakuwa chanzo cha mateso hayo, bali alikuwa akukiuka haki za binadamu kwa njia katili kabisa. Wale waasisi wa fikara ya kuwatesa wafungwa wamekaa bukheri makwao bila ya kuhukumiwa. Kinyume kabisa cha mambo, mshauri wa mambo ya sheria wa Ikulu ya Marekani, Albert Gonzales aliyepinga kutumiwa kwa Mkataba wa Geneva wenye kuhakikisha hifadhi ya mahabusi wa kivita, karibuni ataidhinishwa na Baraza la Senate la Marekani kuwa Waziri wa Sheria."
Na gazeti la VOLKSSTIMME kutoka Magdeburg linahisi kuwa: "Hakuna raiya yeyote wa Kiiraq anayeweza kusahau zile picha za kukereketa za mateso zinazowateremshia heshima yao wafungwa wa Kiiraq katika jela ya Abu Ghuraib. Lakini huenda hukumu ya adhabu iliyopitishwa huko Fort Hood imewatuliza na kuwapa maridhio ya kiadilifu wale mamiliyoni ya Wairaq wanaoendelea kutatizwa na wimbi la mapigano ya itikadi kali, wenye kulilia amani. Mahakama ya kijeshi ya Kimarekani imeonyesha wazi wazi kuwa kabisa haiko tayari kuvumilia au kusamehe mateso ya wafungwa wa Kiiraq. Hatimaye hukumu hiyo imeweka misingi inayopiga marufuku ukiukaji wa haki za binadamu iliyokuwa isisitizwe tangu mwanzo katika hali ya vita vya Iraq."
Baada ya kugunduliwa chembe-chembe za sumu ya Dioxine katika kuku wanaofugwa huru mashambani, naye Waziri Mambo ya Kilimo, Renate Künast ameanza kulaumiwa: Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE kutoka Potsdam linaandika:
"Mabingwa – na hata wale wasiofahamu vipengele vya biashara ya kuku, mara kwa mara wakisisitiza kuwa kwa mtazamo wa afya ya vyakula, yai linalotagwa na kuku wanaofugwa kwa maelfu katika mabanda ya viwanda vya kilimo ni afadhali kupita yai linalotagwa na kuku wanaofugwa huru mashambani wanaoathiriwa na kila aina ya sumu zinazochafua mazingira. Kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Kilimo Renate Künast muda mrefu amekataa kabisa kulisikiliza lalamiko hilo, sasa hana budi kulaumiwa. Baada ya kugunduliwa chembe-chembe hizo za sumu ya Dioxine, sekta nzima ya ufugaji huru wa kuku imeanza kujipatia sifa mbaya, na Waziri Künast atakutana na shida ya kuendelea kutetea kisiasa msimamo wake wa kupinga kila aina ufugaji wa kuku wanaotagishwa mayai katika mabanda makubwa ya makampuni ya kilimo."