UEFA EURO 2012: Uhispania ndani ya nusu fainali
24 Juni 2012Dimba hilo kufikia sasa limedhihirisha ubora wa hali ya juu, kabumbu la kusisimua lakini kwa ujuzi wa Uhispania kuuweka mpira miguuni na pasi zao fupi fupi za uhakika, nafasi za kufunga bao katika uwanja wa Donesk zilikuwa chache.
Mabingwa wa ulimwengu Uhispania kwa mara nyingine walianza bila shambulizi na likawa jukumu lake kiungo Xabi Alonso kufunga bao la ufunguzi kwa kichwa katika dakika ya 19 kwenye mchezo wake wa mia moja wa kimataifa wakati vijana hao wa Vicente del Bosque kwa mara ya kwanza kuvunja ngome na kupiga krosi safi.
Bao hilo lilikuwa la 20 ambalo ni rekodi katika dimba la UEFA EURO na mchezaji huyo wa Real Madrid akaongeza la pili kwa njia ya penalti katika dakika za mwisho mwisho.
Alonso alisema kikosi kilicheza vizuri na yeye binafsi aliridhika na mabao hayo mawili. Aliongeza kuwa hawakuwa na nafasi nyingi lakini waliudhibiti mchuano huo.
Ushindi wa Uhispania ambao ni wa kwanza katika mechi ya ushindani dhidi ya Ufaransa, ulikuwa na maana kuwa kinyang'anyiro hicho kilishika kasi baada ya Ujerumani wanaopigiwa upatu kuwafunga Ugiriki magoli manne kwa mawili katika mchuano wa kusisimua zaidi wa robo fainali siku ya Ijumaa.
Uingereza kuumana na Italia
Katika mchuano wa leo usiku, Uingereza itajaribu kufika katika awamu ya nne bora ya kinyang'anyiro cha kikuu kwa mara ya kwanza katika miaka 16 wakati itakapokabana koo na Italia katika mchuano mkubwa wa robo fainali.
Ujasiri na matumaini yaliyomo ndani ya kikosi chipukizi cha kocha Roy Hodgson yanatokana na ukweli kwamba Uingereza haijawahi kufuzu katika robo fainali ya mashindano makuu.
Lakini baada ya kushinda kundi D mbele ya Ufaransa na kuendeleza mbinu zao za ushindi kwa mechi ya tano mfululizo, Uingereza inaingia katika mchuano huo mjini Kiev ikiwa na imani kuwa inaweza kusalia katika dimba hilo.
Kitu kinachomsumbua kichwa Hodgson ni kwamba wachezaji wake watano muhimu wanakabiliwa na hali ngumu ya kujikuta katika adhabu ya kinidhamu kabla ya mchuano huo.
Steven Gerrard, Ashley Cole, Ashley Young, James Milner na Alex Oxlade-Chamberlain wanakodolewa na hatari ya kukosa uwezekano wa mchuano mkali wa nusu fainali dhidi ya Ujerumani, ikiwa watapata kadi moja ya njano kila mmoja.
Kocha wa Italia Cesare Prandelli wakati huo huo amelazimika kuifanyia mabadiliko safu yake ya ulinzi kufuatia jeraha lililompata Beki wa kati Giorgio Chiellini ambaye huenda akabadilishwa na Leonardo Bonucci.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri:Josephat Charo