UEFA EURO 2012 yaanza
8 Juni 2012Lakini wakati mamilioni ya wapenzi wa soka wakitarajiwa kuburudishwa na uhondo wa tamasha hilo ambalo ndilo maarufu zaidi miongoni mwa mashabiki wa Ulaya, kunayo hofu ya kuchafuliwa na visa vya ubaguzi.
Hata kabla ya kipyenga cha kuanza michuano kupulizwa, tayari kuna madai ya kutokea visa vya ubaguzi wa rangi katika dimba la UEFA EURO 2012 linaloandaliwa Poland na Ukraine. Nahodha wa timu ya taifa ya Uholanzi Mark van Bommel amesema katika mahojiano yaliyochapishwa leo kwamba timu yake ilisikia nyimbo za kibaguzi wakati ikifanya mazoezi ya kikosi mbele ya mashabiki katika mji wa kusini mwa Poland, Krakow.
Uholanzi yalalamika
Van Bommel amenukuliwa na gazeti la De Telegraf akisema kuwa wote walisikia nyimbo za kumwiga tumbili, na hawawezi kukubali hilo. Kiungo huyo wa klabu ya AC Milan aliongeza kuwa ikiwa tukio kama hilo litatokea wakati wa kinyang'anyiro, watamwendea mwamuzi wa mechi mara moja na kumwomba aingilie kati.
Afisa mmoja mkuu wa shirika la soka la Ulaya UEFA aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kundi dogo la waandamanaji liliulenga uwanja wa mazoezi unaotumiwa na timu ya Uholanzi mjini Krakow siku ya Jumatano lakini akakanusha kuwa maandamano hayo yalikuwa ya kibaguzi.
Rais wa UEFA Michel Platini amewataka waamuzi wa mechi kuzuia au hata kusitisha michuano ikiwa wachezaji watabaguliwa na mashabiki. Shirikisho hilo limemteua refa Muitaliano Nicola Rizzoli kuamua mchuano wa hisia kali kati ya Uingereza na Ufaransa mjini Donetsk mashariki mwa Ukraine siku ya Jumatatu.
UEFA imewaeleza waamuzi wa mechi 12 jinsi ya kushughulikia nyimbo za kibaguzi na ishara kutoka katika maeneo ya viti vya mashabiki.
Mafanikio ya wenyeji
Naye rais wa Ukraine aliwataka wananchi wake kuwakaribisha wageni kwa moyo mkunjufu wakati wa dimba hilo. Rais Viktor Yanukovych alisifu mafanikio yaliyopatikana katika kuandaa kinyang'anyiro hicho. Alipongeza nchi hiyo kwa kujenga barabara, viwanja vya michezo na ndege kwa ajili ya UEFA EURO 2012.
Katika mechi za leo mbili za ufunguzi Wenyeji Poland watafungua dimba dhidi ya Ugiriki kabla ya Jamhuri ya Czech kujitosa uwanjani kuvaana na Urusi.
Wakati huo huo Uingereza imesema kuwa haitawatuma mawaziri wowote katika mechi za awamu ya makundi. Ofisi ya mambo ya kigeni ya Uingereza imesema hakuna maafisa wa ngazi za juu watakaohudhuria mechi za awamu hiyo huku kukiwa na ripoti za kufungwa jela Waziri Mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko. Nchi kadhaa za Ulaya ikiwemo Ufaransa na Austria tayari zimetishia kususia dimba hilo zikitaja ripoti za unyanyasaji wa kiongozi huyo wa Upinzani nchini Ukraine aliye gerezani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu