1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA EURO 2012

Josephat Nyiro Charo12 Juni 2012

Sheva aipa ushindi Ukraine huku Ufaransa ikitoka sare na England. Ushindi wa Ukraine unaiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika robo fainali.

Ukraine's Andriy Shevchenko, left, scores his side's second goal during the Euro 2012 soccer championship Group D match between Ukraine and Sweden in Kiev, Ukraine, Monday, June 11, 2012. (Foto:Darko Vojinovic/AP/dapd)
Shevchenko akifunga bao la ushindi la UkrainePicha: dapd

Michauno ya kombe la mataifa ya Ulaya ilianza kwa mtindo wa kipekee kwa wenyeji Ukraine wakati walipoichapa Sweden mabao 2-1, huku mshambuliaji matata Andriy Shevchenko 'Sheva' akifunga mabao yote mawili maridadi kabisa kukamilisha siku njema kwa waandaaji hao wenza wa michunao ya UEFA EURO 2012 katika kundi D.

Zlatan Ibrahimovic aliifungia Sweden goli la pekee dakika saba baada ya kipindi cha mapumziko. Kisha baadaye mchezaji nyota wa zamani wa timu ya Milan, Shevchenko mwenye umri wa miaka 35 aliwasazisha dakika tatu baada ya bao la Ibrahimovic na kisha kupachika bao la ushindi dakika ya 68 ya mchezo.

Ibrahimovic akiutikisa wavu wa UkrainePicha: Reuters

Baada ya mechi hiyo Schevchenko alisema anahisi ni kama ana umri wa miaka 20 na wala sio 35. "Tuna nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hii. Najisikia vizuri. Ulikuwa mchuano wa kihistoria kwetu. Ni ushindi wa kihistoria," aliongeza kusema Schevchenko.

Kocha wa Sweden, Erik Hamren hajaridhishwa na matokeo hayo. Amesema ili kushinda mechi zao wanahitaji wachezaji 11 waonyeshe mchezo wa hali ya juu kabisa. "Leo pengine watano au sita walionyesha ujuzi ninaoutaka. Hiyo haitoshi," akaongeza kusema kocha huyo.

Ufaransa yatoka sare na England

Kwenye mechi ya kwanza ya kundi D, England ilitoka sare ya 1:1 dhidi ya Ufaransa. Mkwaju wa 'freekick' uliopigwa na Steven Gerrard baada ya mwenzake James Milner kufanyiwa madhambi na Patrice Evra wa Ufaransa, ulipachikwa wavuni na Joleon Lescott kwa kichwa dakika ya 30 ya mpambano huo. Samir Nasri aliutikisa wavu wa England na kusawazisha dakika chache baadaye.

Bao la Nasri lilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi kuliko kusawazisha tu kwa sababu limeisaidia Ufaransa kuepuka aibu nyengine baada ya balaa la michuano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na michunao ya kufuzu kwa EURO 2008 ambapo wachezaji walirejea nyumbani wakiwa na aibu baada ya kutolewa kwenye raundi ya kwanza.

Nasri (kushoto) akijiandaa kufunga baoPicha: picture-alliance/dpa

Nasri mwenyewe amesema ana imani wanayo nafasi nzuri katika michuano ya mwaka huu na lengo lao ni kufika robo fainali. "Hatujapoteza kwa hiyo ni muhimu kuzingatia mpambano wetu dhidi ya Ukraine siku ya Ijumaa."

Kocha wa Ufaransa, Laurent Blanc, amesema hawajafurahishwa sana na matokeo ya mechi hiyo lakini hawajavunjika moyo. "Tungepoteza mechi hii kama hatungejitahidi, lakini ukiangalia kwa ujumla tumecheza vizuri zaidi kuliko England," ameongeza kusema kocha huyo. Naye kocha wa England, Roy Hodgson kwa upande wake amesema mechi ilikuwa ngumu lakini wameridhika na matokeo.

Ufaransa sasa itachuana na Ukraine ambayo iko katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa robo fainali huko Donetsk Ijumaa ijayo. England kwa upande wao wataumana na Sweden.

Poland kuumana na Urusi

Katika michuano ya leo ya kundi A, Ugiriki inarudi uwanjani kumenyana na Jamhuri ya Cheki huku wenyeji Poland wakipambana na Urusi katika uwanja wa mjini Warsaw. Mji huo unakabiliwa na kile ambacho maafisa wamekitaja kuwa changamoto kubwa kabisa ya usalama, Poland ikicheza na mahasimu wake wa zamani Urusi katika mechi inayolazimika kushinda.

Miongo kadhaa ya uhusiano mbaya na kutiliana shaka kati ya nchi hizo na baadhi ya mashabiki wa pande hizo kuwa na sifa za kuzusha vurugu, kumesababisha wasiwasi huenda kukatokea mapambano hata kabla ya mechi hiyo kuanza. Lakini mechi ya kirafiki kati ya mashabiki wa Urusi na Poland iliyopangwa kuchezwa saa sita mchana inatoa ujumbe wa amani. Hatua nyengine muhimu imechukuliwa jana wakati mashabiki kutoka pande zote mbili walipoweka mashada ya maua kuwaenzi Wapoland na Warusi waliouawa wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/REUTERS

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW