UEFA EURO 2020 kuandaliwa kote Ulaya
16 Novemba 2012Platini amesema katika mahojiano na gazeti la Ijumaa hapa Ujerumani The Bild kwamba wazo lake ni kuleta dimba la UEFA EURO kwa watu na siyo watu kwa dimba hilo, na kwamba kuandaa dimba hilo katika mataifa kadhaa ni rahisi kufanikisha katika wakati huu mkuu wa kiuchumi. Mpango huo uliwasilishwa kwanza na Platini katika fainali za UEFA EURO 2012, ukitaka mechi za kinyang'nyiro hicho zichezwe katika miji 13 ya Ulaya. Miji 12 itaandaa mechi za awamu ya makundi, na awamu y akwanza ya muondowano, kwa kuzingatia kufuzu kwa timu zinazoshiriki pamoja na orodha ya msimamo wa FIFA. Mji wa kumi na tatu, ambao Istanbul inasemekana kujipigia debe, utaandaa mechi za nusu fainali na fainali ya hafla hiyo inayozishirikisha timu 24. baadhi ya mashirikisho ya soka yameliunga mkono wazo hilo huku wawakilishi wa mashabiki wakihofia ukosefu wa mazingira ya msisimko katika viwanja na pia gharama za juu za kusafiri.
Aliyekuwa meneja mkurugenzi wa klabu ya Werder Bremen Klaus Aloffs amesaini mktaba wa miaka minne kuwa mkurugenzi wa spoti wa mahasimu wao wa Bundesliga VfL Wolfsburg. Aloffs amesaini mkataba hadi mwkaa wa 2016 na ana jukumu la kuwaondoa Wolfsburg kutoka eneo la kushushwa daraja. Wakati akiwa meneja wa Bremen, Allofs alishinda taji la Bundesliga mwaka wa 2004 na mataji mawili ya kombe la shirikisho Ujerumani mwaka wa 2004 na 2009 kwa ushirikiano na kocha Thomas Schaaf.
Nyota wa Hoffenheim Boris Vukcevic, ambaye alijeruhiwa vibaya wakati gari lake lilipogongana na lori mwezi Septemba, amepata fahamu jana asubuhi ikiwa ni wiki saba baada ya kukosa fahamu. Meneja wa klabu hiyo amesema wana furaha kuwa hali ya Boris inaendelea kuimarika, na wkamba wanamwombea kila siku. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alipata majeraha mabaya ya kichwa katika ajali hiyo.
Arjen Robben arudi mkekani
Katika habari nyingine za Bundesliga ni kuwa mshambuluaji wa Bayern Munich Arjen Robben ametemwa katika mechi zijazo za klabu hiyo za Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kupata jeraha dogo la msuli katika mchuano wa kirafiki wa kimataifa Jumatano iliyopita.
Robben alikuwa amerejea majuzi baada ya kuwa nje kwa wiki nne kutokana na jeraha la mgongo na amekosa mchuano wa leo dhidi ya Nuremberg pamoja na atakuwa nje wiki ijayo katika mchuano wa ligi ya mabinwga dhidi ya Valencia.
Mikakati ya AFCON 2013
Waamuzi watakaosimamia mechi za kombe la mataifa ya bara Afrika mwaka wa 2013 nchini Afrika Kusini watatengwa na umma wakati wa dimba hilo mwaka ujao ili kuepuka sakata za kupanga mechi. Afisa Mkuu Mtendaji wa Kamati andalizi ya fainali hizo Mvuso Mbebe ameiambia kamati ya bunge ya Afrika Kusini kuwa waandalizi watatekeleza hatua sawa za usalama jinsi tu ilivyokuwa wakati wa mechi za dimba la dunia mwaka wa 2010.
Sasa tuangalie soka ya Afrika ambapo Marefa wataishi katika hoteli ambazo hakuna mtu yeyote atakayekutana nao. Polisi watawasindikiza marefa kutoka vyumba vyao vya hoteli hadi viwanja vya michezo. Ofisa huyo amesema hatua hiyo imeidhinishwa na shirikisho la soka Afrika CAF. Kinyang'anyiro hicho cha AFCON kinaanza tarehe 19 Januari hadi tarehe 10 Februari mwaka wa 2013.
Mwandishi : Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman