1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufanisi mdogo katika ushirikiano kati ya Boko Haram na IS

7 Machi 2016

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alitangaza kulitii kundi la Dola la Kiiislamu lakini hakuna ufanisi mkubwa unaoonekana katika ushirikiano kati ya makundi hayo mawili.

Abubakar Shekau
Kiongozi wa kundi la Boko Haram, Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Wakati kundi la Boko Haram lilipotangaza kulitii kundi la Dola la Kiislamu IS nchini Iraq na Syria mwaka jana, kulikuwa na hofu uasi wa umwagaji damu kaskazini mashariki mwa Nigeria ungetokea katika kiwango cha kimataifa, kwa kuwa makundi hayo ya kigaidi yalikuwa yameungana rasmi. Lakini wachambuzi wanasema hakuna ufanisi mkubwa unaoonekana kutokana na ushirikiano kati ya makundi hayo.

Kufuatia tangazo la kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau kulitii kundi la Dola la Kiislamu miezi 12 iliyopita, kulizuka hofu na wasiwasi kwamba wapiganaji wa kigeni wangemiminika katika mataifa yanayolizunguka ziwa Chad na kuuchochea mzozo ambao awali ulikuwa wa kikanda. Lakini hilo mpaka sasa halijatokea.

Kiongozi wa kundi IS, Abu Bakr al-BaghdadiPicha: picture-alliance/AP Photo

Kundi la Boko Haram linaonekana kuwa dhaifu na limesambaratika baada ya operesheni ya kijeshi dhidi yake iliyodumu mwaka mmoja. Shekau amesikika mara mbili tu tangu alipotoa ujumbe wa sauti Machi 2, 2015 akiahidi kumtii kiongozi wa kundi la Dola la Kiislamu, Abu Bakar al-Baghdadi.

Jeshi la Nigeria limefaulu kuwachakaza wanamgambo wa Boko Haram na kuzishambulia ngome zao na kuwakomboa maelfu ya watu wanaoishi chini ya udhibiti wa kundi hilo. Wiki iliyopita, wapiganaji kadhaa walijisalimisha kwa sababu ya njaa. Nigeria sasa inataka watu milioni mbili waliolazimika kuyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi nchini mwao, warejee nyumbani.

Hakuna kilichobadilika baada ya tangazo

Wachambuzi wengi wamelitazama tangazo la ushirikiano kama propaganda kwa pande zote mbili. Kundi la Boko Haram wakati huo lilikuwa likipambana na vikosi vya kikanda na Dola la Kiislamu likikabiliwa na changamoto katika azma yake ya kutanua himaya yake.

"Hakuna kilichobadilika katika kambi ya Boko Haram tangu tangazo la Shekau," amesema mchambuzi wa masuala ya usalama wa Nigeria Abdullahi Bawa Wase.

Akizungumza na shirika la habari la AFP Wase alisema tangazo hilo limeshindwa kuwaleta wapiganaji wa Dola la Kiislamu. Limeshindwa kuvutia silaha na fedha za kundi la IS, jambo ambalo wengi walihofia lingetokea. Lakini kinyume kabisa na matarajio, kundi la Boko la Haram ni dhaifu kuliko lilivyokuwa kabla ya tangazo hilo, ukweli unaodhihirika kutokana na kupungua kwa mashambulizi kwa kiwango kikubwa. Hata kasi ya mashambulizi ya kujitoa muhanga imepungua.

Shambulizi la Boko Haram, kijiji cha Dalori, kilometa 5 kutokak Maiduguru, 31.01.2016Picha: picture alliance/AP Photo/J. Ola

Duru ya usalama nchini Nigeria imesema Dola la Kislamu ni nembo ya kutangazia bidhaa ambayo Boko Haram inataka kuitumia kujionesha kama kundi thabiti la kigaidi.

Tangazo la Shekau na hatua ya kuligeuza jina la Boko Haram kuwa Dola la Kiislamu Afrika Magharibi, Islamic State West Africa Province, ISWAP, lilisababisha mpasuko katika uongozi wa kundi hilo. Viongozi wachache, kama walikuweko, walitaka kuipinga kauli yake, lakini wapinzani wametafuta uwezekao wa ushirikiano wa karibu na makundi mengine ya jihadi katika eneo pana la Sahel.

Boko Haram kugeuzwa kuwa kitisho cha kikanda

Baadhi ya washauri wa masuala ya usalama wanabashiri Boko Haram nchini Nigeria huenda mwaka huu ikadhibitiwa na kuwa kitisho cha kihalifu cha kanda kama vile kundi la Lord's Resistance Army, LRA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Lakini baada ya Marekani kuiingiza Nigeria katika orodha yake ya "Worldwide Caution" - "Tahadhari Duniani Kote", serikali za mataifa ya Magharibi zinaendelea kuliona kundi la Boko Haram kama kitisho. Ndege zisizo rubani za Marekani hivi karibuni zilianza kufanya kazi kutoka kambi moja kaskazini mwa Cameroon huku wizara ya ulinzi Pentagon ikitafakari kupeleka wakufunzi wa kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, ambaye amedai Boko Haram imeshindwa kiufundi, ameendelea kuitaja Libya kuwa ni kitisho cha usalama kwa bara la Ulaya na Afrika akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.

Rais wa Nigeria, Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/dpa/W. Krumm

Yan St-Pierre, mtaalamu wa Shirika la Ushauri wa Usalama, Modern Security Consulting Group (MOSECON), alisema hapana shaka kwamba kundi la Boko Haram limekuwa likiwasiliana na makundi mengine ya jihadi kwa biashara na vifaa katika mwaka uliopita. "Kwa kuwa inadhaniwa wapiganaji wa Afrika Magharibi na mataifa ya Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara wanaoendesha shughuli zao nchini Libya wameondoka, makundi tofauti tofauti katika eneo hilo yamekuwa yakishirikiana kutoa fedha, vifaa na wapiganaji," aliongeza kusema mtaalamu huyo.

Yan St-Pierre alisema katika barua pepe inaaminika kwamba kundi la al Qaeda katika eneo la Maghreb, AQIM, na makundi madogo madogo ya Boko Haram yanaongeza ushirikiano wao, licha ya kwamba kundi la Boko Haram limetangaza rasmi utiifu wake kwa kundi la Dola la Kiislamu.

"Lakini licha ya mafungamano hayo, Nigeria haionekani kuwa nchi inayolengwa kwa sasa," amesema Ryan Cummings, mtaalamu wa masuala ya usalama barani Afrika. "Ninaamini kabisa kwamba kama ushirikiano kati ya Boko Haram na Al Qaeda katika eneo la Maghreb ungekuwepo, kungekuwa na ushahidi wa wazi zaidi wa ushirikiano huu," akaongeza kusema Cummings.

Cummings pia alisema kuwa katika tamko la hivi karibuni la Dola la Kiislamu, uongozi wa kundi hilo unadaiwa kuwaomba wafuasi wao katika eneo la Sahel na Maghreb kwenda Libya kusaidia operesheni za mapambano badala ya kwenda kulisaidia kundi la Boko Haram katika bonde la ziwa Chad.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe

Mhariri:Sudi Mnette