1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kidedea dhidi ya Romania

Admin.WagnerD11 Juni 2016

Fainali za mwaka huu za Kombe la mataifa ya Ulaya, Euro 2016, zimefunguliwa rasmi usiku wa kuamkia leo Jumamosi(11.06.2016) nchini Ufaransa, kwa mechi kati ya wenyeji Ufaransa na Romania katika uwanja wa Stade de France.

UEFA EURO 2016
Sherehe za ufunguzi wa michuano ya Euro 2016 mjini ParisPicha: Reuters/C. Platiau

Ufaransa imeanza vizuri mashindano haya ya kombe la mataifa ya Ulaya jana Ijumaa , kwa timu yake ya taifa kuishinda Romani kwa mabao 2-1 na majeshi ya usalama yakisimama imara na kuhakikisha kwamba kila mtu anakuwa salama katika viwanja na mitaani ambako mashabiki walisheheni katika maeneo mbali mbali wakiangalia mtanange huo.

Olivier Giroud akishangiria bao la kwanza kwa UfaransaPicha: Reuters/C. Hartmann

Miezi saba baada ya uwanja wa mpira kulengwa katika mashambulizi ambayo yalisababisha watu 130 kuuwawa mjini Paris, taifa hilo wenyeji wa Euro 2016 lilifungua mashindano hayo yanayoshirikisha timu 24 kwa bao la dakika za mwisho na kuishinda Romania kwa mabao 2-1.

Majeshi ya usalama katika mji wa Marseille hayakuwa na kazi rahisi hata hivyo. Mabomu ya kutoa machozi yalirindima dhidi ya mashabiki wakorofi kwa siku ya pili mfululizo kabla ya mpambano wa Uingereza dhidi ya Urusi leo jioni(10.06.2016), na kuleta kumbumbuku zisizo pendeza za ghasia zinazowahusisha mashabiki wa Uingereza katika mji huo wa pwani ya kusini mwa Ufaransa, wakati wa kombe la dunia mwaka 1998.

Wachezaji wa Ufaransa wakimkumbatia Dimitry Payet baada ya kufunga bao la pili kwa UfaransaPicha: Reuters/C. Hartmann

Kumbukumbu isiyosahaulika

Kwa Dmitry Payet , hata hivyo, siku ya jana Ijumaa (10.06.2016) ilikuwa ya kumbukumbu kubwa. Mchezaji huyo wa kati wa Ufaransa alimimina krosi ambayo Olivier Giroud aliiweka wavuni kwa kichwa katika dakika ya 58 na kufunga bao la kwanza katika fainali hizi za mwaka huu na kisha Payet binafsi alipachika bao la ushindi baada ya Bogdan Stancu kusawazisha kwa Romania kwa mkwaju wa penalti.

Mashabiki wa Romania katika uwanja wa Stade de FrancePicha: Reuters/D. Staples

Licha ya kwamba alicheza msimu wake bora kabisa akiwa na West Ham United nchini Uingereza, Payet alipata taabu kuweza kuamini alichokifanya katika dakika ya 89, na alibubujikwa na machozi wakati akitoka uwanjani baada ya kocha Didier Deschamps kuamua apumzike.

"Iwapo mtu angeniambia mambo yangekwenda yalivyokwenda nisinge amini ," amesema Payet.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alimsifu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye aliitia nguvu timu yake wakati ikitafuta kwa udi na uvumba kutaka kupasua ngome ya Romania.

"Ana uwezo wa kufanya vitu ambavyo ni adimu ," Deschamps amesema. "Lilikuwa ni goli zuri sana."

Mashabiki wa UfaransaPicha: Reuters/D. Staples

Mnara wa Eiffel

Wakati mchezo kati ya Ufaransa na Romani ulipomalizika , mnara wa Eiffel uliwashwa taa za rangi ya bendera ya taifa la Ufaransa. lakini sherehe katika mnara huo ambao ni alama ya kihistoria ya nchi hiyo hazikuweza kulingana na shangwe ya mashabiki chini ya mnara huo.

"Nimefarijika , ulikuwa mchezo wenye mbinyo mkubwa," amesema Alexandre Robert , mwenye umri wa miaka 26, alijifunika bendera ya Ufaransa huku akijichora rangi tatu ta bendera hiyo katika mashavu yake. Nyuma yake , makundi ya watu walicheza, wakiimba na kukumbatiana.

Mashabiki wa Uingereza wakipambana na polisi mjini MarseillePicha: Getty Images/L. Neal

Kocha wa Romani Anghel Iordanescu ameonya kwamba itakuwa vigumu kwa wachezaji wake waliochoka kuweza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kushindwa kwa bao la dakika za mwisho dhidi ya Ufaransa katika mchezo huo wa ufunguzi.

Iordanescu hata hivyo amefurahishwa na juhudi za kikosi chake, kwa jinsi walivyowabana wenyeji na moja ya timu zinazopigiwa upatu kutoroka na taji hilo mwaka huu na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao licha ya kushindwa katika mchezo wa jana. Jioni ya leo mtanange unaendelea ambapo mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Albania na Uswisi , kisha Wales itaingia uwanjani kupambana na Slovakia na kisha Uingereza itapambana na Urusi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi / Sekione Kitojo


Mhariri: Mohammed Khelef