Ufaransa kumshitaki mwanajeshi wa zamani wa Rwanda
9 Aprili 2026
Mahakama ya Ufaransa itamshtaki luteni kanali wa zamani wa jeshi la Rwanda Cyprien Kayumba kwa mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya kimbari kwa madai ya kuwasilisha silaha zilizotumika wakati wa mauaji ya mwaka 1994.
Hayo ni kwa mujibu wa chanzo cha mahakama katika kauli yake ya jana Jumatano.
Kayumba mwenye umri wa miaka 71 kutoka kwa jamii ya Wahutu, aliongoza idara ya wizara ya ulinzi iliyohusika na kuagiza na kuwasilisha silaha wakati wa mauaji ya kimbari.
Kayumba, ambaye ameishi Ufaransa tangu 1998, amekuwa akidai kila mara kwamba hakujua silaha alizoagiza zingetumika kuwaua Watutsi.
Majaji waliamuru kwamba Kayumba ashtakiwe katika tarehe ambayo haijapangwa kwa mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya kimbari na kushiriki katika uhalifu dhidi ya binadamu. Walimwamuru akabidhi pasipoti yake na kumkataza kuondoka Ufaransa.