Ufaransa kuumana na Iceland robo fainai
1 Julai 2016Matumaini ya Iceland yako juu sana lakini wanafahamu kuwa timu nyingine sasa zitawachukulia kwa umakini zaidi. Ufaransa watalenga kuonyesha mchezo wa kuridhisha na sio kutoka kijasho kama ilivyokuwa katika dimba hili. Les Bleus walishinda Euro 1984 na Kombe la Dunia 1998 katika ardhi ya nyumbani. Patrice Evra ni beki wa Ufaransa "Tunastahili kujiambia, “ni mechi muhimu”, tunapaswa kutinga nusu fainali. Tuko nyumbani, haitakuwa rahisi, tutastahili kujituma sana. Natumai hatutachanganyikiwa bali tutacheza vyema. Bila shaka najiwekea mwenyewe shinikizo. Kwangu mimi, kutofuzu hatua hii, ntajihisi kuwa nimekwama na sitaki hilo.
Taifa zima linataka ushindi kutoka kwa vijana hao wa Didier Deschamps lakini Iceland haipaswi kupuuzwa hasa baada ya timu hiyo ndogo kuiduwaza England kwa kuibandua nje katika hatua ya mchujo. Huyu hapa Evra "Wamecheza pamoja kwa miaka minne au mitano, wana wachezaji wazuri sana. Nilimpenda namba nane wao ambaye hakuupoteza mpira hata kidogo, nnaiheshimu sana timu hii. Wanajua namna ya kupiga pasi, kuudhibiti mpira. Nawaheshimu wapinzani wetu wote.
Iceland wamesaliwa kuwa watulivu hasa ikizingatiwa kuwa hii ni mara yao ya kwanza kushiriki katika dimba hili na isitoshe wamefika katika hatua ya robo fainali. Birkir Bjarnsson ni kiungo wa Iceland "Kwetu huenda ni mchuano mkubwa sana katika historia yetu. Kupambana na Ufaransa, nchini Ufaransa ni safi sana. Mazingira na vitu vyote vinavyouzunguka mchuano huu vitakuwa sawa kabisa na nadhani wachezaji watafurahia.
Kocha mwenza wa Iceland Heimir Hallgrimsson anasema wachezaji wake wanaendelea kuimarika na anatumai mwenendo huo utaendelea dhidi ya Ufaransa "Tumekuwa tukicheza vizuri sana tangu mwanzo wa dimba hili hivyo natumai mchezo wetu bora zaidi haujafika. Tunajivunia sana wachezaji wetu kwa sababu wameonekana kuimarika katika kila mchezo tuliocheza. Tutumai kuwa tutaendelea kukua katika kila mchezo tuliobaki nao katika dimba hili
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef