Ufaransa kuumana na Ureno katika fainali
8 Julai 2016Fainali ya mashindano hayo yaliyodumu kwa mwezi mmoja inamkutanisha mfungaji mabao mengi katika dimba hilo kwa Ufaransa Antoine Griezmann na nyota wa Ureno Cristiano Ronaldo ambaye anataka kushinda kombe na timu ya taifa ili kuongeza kwenye mataji yake ya klabu.
Ufaransa wameridhisha zaidi katika mchezo wao kuliko Ureno na wanapigiwa upatu hasa kutokana na rekodi ya takwimu za mchezo kati ya timu hizo mbili, ambapo wameshinda 18 kati ya mechi 24 na kushindwa tano pekee, wa mwisho ukiwa katika mchuano wa kirafiki mwaka wa 1975.
Iwapo watashinda taji hilo kesho basi watajiunga na Uhispania na Ujerumani katika nchi zenye rekodi ya mataji matatu
Timu zote zinaonekana kuwa thabiti lakini Ufaransa bila shaka ina idadi kubwa ya wachezaji nyota kama vile Griezmann, Paul Pogba, Dimitri Payet, Olivier Giroud na Patrice Evra. Ureno watawategemea nahodha Cristiano Ronaldo, Nani, chipukizi Renato Sanches, na mabeki Pepe na William Carvalho.
Ni ipi hatima ya Loew baada ya Euro 2016
Kocha wa timu ya Ujerumani Joachim Loew amekataa kusema kama atabakia katika wadhifa huo baada ya kukamilika dimba lijalo la Kombe la Dunia. Baada ya mabingwa hao wa dunia kuduwazwa na mabao mawili ya Antoine Griezmann yaliyofikisha kufikisha kikomo safari yao nchini Ufaransa, Loew aliulizwa kama ananuia kubakia baada ya Kombe la Dunia la 2018 nchini Urusi…Loew alijibu kuwa na namnukuu “bado nimesikitika kupoteza nusu fainali dhidi ya Ufaransa hivyo sitaki kufikiria kuhusu hilo usiku huu”. Jinsi ntakavyokabiliana na hilo ni vigumu kujibu, hatukujadili hapo kabla cha kufanya baada ya kichapo, tutazungumzia hilo katika siku chache zijazo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef