Ufaransa: mashambulizi ya Paris yalipangwa Syria
16 Novemba 2015Waziri mkuu wa Ufaransa Manuell Valls ameonya kuwa nchi nyingine za Ulaya pia zinakabiliwa na kitisho cha kushambuliwa na magaidi na kuongeza kuwa wanafahamu kuwa mipango ya kufanya mashambulizi ilikuwa inapangwa na bado inapangwa sio tu kuishambulia Ufaransa, bali nchi nyingine za Ulaya.
Valls amesema kizazi hiki cha sasa kitaishi kwa muda mrefu na kitisho cha ugaidi lakini lazima maisha yaendelee licha ya kuwepo kitisho hicho cha ugaidi.
Hayo yanakuja huku Ufaransa ikifanya mashambulizi ya angani dhidi ya ngome za wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS mjini al Raqqa nchini Syria.
Ufaransa yaishambulia IS
Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema mashambulizi hayo yanahusisha ndege ishirini za kijeshi na zimeangusha mabomu 20 na kuharibu bohari la kuhifadhia silaha na kambi ya kutoa mafunzo ya wanamgambo hao wa IS.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema Ufaransa ina haki ya kuchukua hatua dhidi ya IS baada ya mashambulizi ya Paris na kuongeza mashambulizi dhidi ya wanamgambo hao ni hatua ya kisiasa.
IS imedai kuhusika katika mashambulizi ya Paris ambayo yamewaua kiasi ya watu 129 na kuwajeruhi watu wengine 350.
Polisi nchini Ufaransa imewakamata watu watano katika mji wa kusini mashariki mwa Ufaransa wa Lyon na kukamata chombo cha kurushia maroketi miongoni mwa silaha nyingine.
Misako pia imefanya katika mji wa Toulouse ambapo watu 13 wamekamatwa na msako pia umefanywa katika mtaa wa Bobigny kaskazini mashariki mwa Paris leo asubuhi.
Gazeti la Le Monde limeripoti kuwa mmoja wa washukiwa wa mashambulizi ya Paris alisimamishwa na polisi akiendesha gari kaskazini mwa Ufaransa lakini hakukamatwa. Salah Abdeslam mwenye umri wa miaka 26 alisimamishwa akiwa na watu wengine wawili ndani ya gari.
Ublegiji imetoa kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye alikuwa anafahamika na maafisa wa usalama kabla ya mashambulizi hayo ya Paris.
Ndugu yake Brahim Abdelslam mwenye umri wa miaka 31 raia wa Ufaransa na mkaazi wa Ublegiji, alijiripua karibu na ukumbi wa Bataclan usiku wa Ijumaa.
Kaka yao mwingine Mohammed Abdelslam ni miongoni mwa watu saba wanaozuiwa mjini Brussels, Ubelgiji ili kuhojiwa na polisi. Vyombo vya habari vya Ubelgiji vimeripoti kuwa mwanamume anayeaminika alipanga shambulizi lililotibuka la kuwaua askari wa Ubelgiji mwezi Januari mwaka huu ndiye alipanga mashambulizi ya Paris.
Washambuliaji zaidi watambuliwa
Abdelhamis Abaaoud mwenye umri wa miaka 28 raia wa Ubelgiji mwenye asili ya kimorocco anaripotiwa kuwa alikuwa mpiganaji wa IS nchini Syria. Abaaoud ambaye saa hizi hajulikani aliko, alikuwa anakaa katika mtaa wa Molenbeek mjini Brussels, mtaa mmoja na alikoishi Brahim Abdelslam.
Mwendesha mashitaka wa Ufaransa Francois Molins amesema washambuliaji wengine wawili wametambuliwa huku mmoja akisemekana kutokea Syria.
Alama za vidole za mmoja wa washambuliaji walioushambulia ukumbi wa Bataclan zinafanana na za mwanamume kwa jina Ahmad Al Mohammad mwenye umri wa miaka 25 aliyeingia Ulaya kupitia Ugiriki mwezi Okotoba akiwa na pasipoti ya Syria.
Mshambuliaji mwingine aliyetambuliwa ni Samy Amimour mwenye umri wa miaka 28 mzaliwa wa Paris na alikuwa anafahamika na maafisa wa usalama kwa kushukiwa kuwa na uhusiano na magaidi na kibali cha kukamatwa kwake kilitolewa mwaka 2103.
Molins amesema jamaa watatu wa Amimour wanazuiwa na polisi kwa uchunguzi. Kwa jumla washambuliaji watano wa Paris wameshatambuliwa kufikia sasa.
Mwandishi: Caro Robi/dpa/Afp/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman