Ufaransa na Mali zasonga mbele
21 Januari 2013Vyanzo vya kijeshi kwa upande wa serikali ya Mali vinaeleza kuwa magari yenye silaha nzito nzito yameondoka katika mji wa Miono, uliopo kilometa 60 kusini mwa Diabaly, eneo ambalo lipo mikononi mwa jeshi la Mali. Vyanzo mbalimbali vya habari vinaeleza kwamba mji wa Diabaly utaweza kukombolewa kwa ukamilifu pasipo mapigano yoyote katika masaa machache yajayo.
Kwa mujibu wa ripoti za jana jioni sana zinaeleza kuwa rais wa Mali alimshukuru rais wa Ufaransa kwa msaada wake wa kijeshi wa kuwaondoa waasi hao wa Kiislamu katika baadhi ya ngome zao huko katika maeno ya kaskazini pamoja na maeneo ya kati ya Mali.
Wanajeshi 400 wawasili Mali
Kwa mujibu wa taarifa ya Ufaransa kiasi ya wanajeshi 400 kutoka, Nigeria Togo na Benin wameshawasili mjini Bamako tangu jana kwa ajili ya kuongeza nguvu katika lengo lile lile la kuwaondoa waasi nchini humo. Na lile jeshi la Chad ambalo linategemewa sana katika mapambano ya katika maeneo ya jangwa nalo pia limewasili nchini Mali.
Afisa mmmoja wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Mali Monique Doray alielezea hali ya usalama ilivyo tete nchini humo kwa kusema. "Tumezidisha maradufu idadi ya walinzi. Na tumeajiri shirika binafsi la ulinzi. Hali kama hii ya vita hatujawahi kushuhudia nchini Mali. Mivutano ilikuwa ikitokea kila mara lakini kinachotekea hivi sasa ni kingine kabisa. Hapa kuna makundi mengi yanayohusika."
Ufaransa ilianzisha operesheni yake ya kijeshi Januari 11, lakini awali ilikwisha sema kwamba vikosi vya Afrika lazima viongoze operesheni hiyo. Maafisa wa juu kabisa katika eneo la kanda ya Afrika Magharibi wamesema ushiriki wa jeshi la Afrika katika operesheni hiyo utagharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 500.
Misaada zaidi kutolewa
Sambamba na jitihada hizo za Ufaransa na Waafrika wenyewe, mataifa mengine makubwa kama Ujerumani, Canada na Urusi zimetoa ahadi za kusaidia juhudi za kukabiliana na waasi hao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema Urusi imejitolea usafiri kwa wanajeshi na vifaa vingine na Canada imeongeza msaada wake wa kuwasafirisha wanajeshi wa Afrika kuwapeleka nchini Mali.
Ahadi hizo zimetolewa kipindi kifupi baada ya Jumuiya ya Kiuchumi wa Africa Magharibi ECOWAS kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa ikitaka msaada wa haraka wa kifedha na vifaa kwa majeshi ya Afrika katika uwanja wa mapambano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle alijibu maombi hayo kwa ya msaada wa kifedha na kuahidi kusaidia kwa kadiri iwezekenavyo pasipo kutaja kiasi cha fedha ambacho taifa lake litatoa.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef