1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Uhispania kulegeza hatua za karantini

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
10 Mei 2020

Ufaransa na Uhispania kulegeza karantini zilizowekwa kwa ajili ya kupunguza maambukizi ya virusi vya corona. Idadi ya watu walioambukizwa yapindukia milioni nne kote ulimwenguni.

Spanien Coronavirus
Picha: Reuters/J. Medina

Raia wa nchi hizo mbili wanapojiandaa kuanza kufurahia kupunguzwa kwa sheria za kubakia majumbani katika nchi hizo mbili zilizoathirika vibaya na janga la corona..Idadi ya watu walioambukizwa duniani kote yapindukia milioni nne. Watu wapatao 277,000 wamefariki kutokana na COVID -19 ulimwenguni kote

Hatua hiyo ya kulegezwa karantini inayotarajiwa kuanza Jumatatu imesababaisha hisia tofauti huku baadhi ya wakuu wa sehemu za biashara wakielezea hofu yao juu ya kufunguliwa tena maduka. Maya Flandin, meneja wa duka la vitabu kutoka mji wa Lyon amesema ana jukumu kubwa la kulinda afya za wafanyikazi pamoja na wateja wao.

Maafisa wa afya nchini Ufaransa wametahadharisha kwamba janga hilo linaendelea kuwepo na maambukizi bado yanatokea na wamekumbusha juu ya hali ya dharura iliyoongezewa muda hadi Julai 10. Hata hivyo maafisa wa afya nchini Ufaransa wamesema idadi ya watu 80 waliofariki siku ya Jumamosi ni ya chini kabisa ukilinganisha na idadi ya watu waliokufa tangu mapema mwezi huu wa Aprili. Ufaransa inajiandaa kupunguza marufuku kwa harakati za umma iliyowekwa wiki nane zilizopita.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: picture-alliance/dpa/AP/Reuters/G. Fuentes

Nchini Uhispania, karibu nusu ya idadi ya watu wataruhusiwa kutoka majumbani mwao Jumatatu na wataruhusiwa kukusanyika  katika makundi madogo madogo tu. Mikahawa itaweza kutoa huduma wakati nchi hiyo inapoanza kipindi cha mpito baada ya karantini kitakachoendelea chini ya uangalizi hadi Juni.

Hata hivyo hofu ipo ya kuibuka tena kwa virusi vya corona ikiwa vizuizi hivyo vitaondolewa kwa haraka. Mamlaka imesema miji miwili ya Madrid na Barcelona haitahusishwa na kulegezwa kwa masharti hayo katika awamu hii ya kwanza kutokana na miji hiyo kuwa ndio vitovu vya COVID-19 nchini Uhispania.  Waziri Mkuu Pedro Sanchez amekumbusha kwamba virusi vya corona bado havijatokomezwa.

Marekani ambayo inaongoza kwa idadi kubwa ya vifo ulimwenguni, Rais Donald Trump amekosolewa vikali mtangulizi wake Barack Obama aliyeonekana kwenye mkanda uliovuja kwamba Trump hakuushughulikia vyema mgogoro huo na kusababisha hali ya sintofahamu.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, hadi kufikia Jumapili zaidi ya watu 78,000 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na COVID -19 nchini Marekani huku watu zaidi ya milioni 1.3 wakiwa wameambukizwa virusi vya corona.

Karantini na kudorora kwa uchumi, kwa wakati huu, kumesababisha mamilioni ya watu kukosa ajira katika hali ngumu inayoukabili ulimwengu mzima. Hata hivyo pamoja na ongezeko kubwa la vifo, nchi kadhaa za Ulaya zimeonyesha ishara za maendeleo mazuri kutoakana na kuchukua hatua za polepole kuelekea katika hali ya kawaida licha ya kwamba safari hiyo bado ni ndefu.

Takwimu za uchumi wa dunia zinaonyesha kushuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha karibu karne moja kutokana na janga la corona lililo lazimisha biashara kufunga na pia kuvuruga vibaya shughuli za usambazaji. Matarajio ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yamedidimia na limisema lilikuwa na matumaini makubwa katika ulitabiri wake wa hapo awali kwamba uchumi wa dunia ungenawiri kwa asilimia tatu katika mwaka huu. Mkuu wa IMF Kristalina Georgiaieva, ambaye shirika lake linapata maombi kadhaa ya mikopo ya dharura amesema sasa matarajio ya kukua kwa uchumi kwa nchi nyingi yako chini ya tathmini ya IMF kwa mwaka 2020.

Chanzo./AFP

 

     

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW