Ufaransa na Uhispania wataka ratiba kamili ya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina
22 Februari 2010Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa na Uhispania wamesema kuwa Ulaya itashinikiza kuwepo ratiba kwa ajili ya duru ya mwisho ya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Mamlaka ya Palestina. Katika taarifa ya pamoja waliyoitoa kwenye gazeti la kila siku la Le Monde, mawaziri hao wamesema mazungumzo hayo yanapaswa kuzingatia kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner na mwenzake wa Uhispania, Miguel Angel Moratinos wamesema kuwa wanataka kupata tarehe kamili ya kufanyika kwa mazungumzo hayo ya mwisho yatakayojadili masuala mbalimbali yakiwemo kuhusu usalama, mipaka, maji, wakimbizi na Jerusalem. Lakini Waziri Kouchner hakurudia kauli yake ya mwishoni mwa wiki ambapo alipendekeza Ulaya kulitambua taifa huru la Palestina hata kabla haijaafikiana kuhusu suala la mipaka na Israel. Kouchner ambaye alikutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina hapo jana na Moratinos ambaye nchi yake ndio mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, wamesema Ulaya huenda ikawa mwenyeji wa mkutano utakaopendekeza tarehe rasmi ya kufanyika mazungumzo hayo ya amani.
Kauli ya mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa na Uhispania, imeripotiwa na gazeti hilo la Le Monde, mara tu Rais Abbas alipokuwa akitarajiwa kukutana na Rais Nicolas Sarkozy mjini Paris katika siku ya pili ya ziara yake. Jana Kouchner alisababisha mgongano mdogo wa kidiplomasia pale alipopendekeza katika mahojiano kwenye gazeti kuwa Ulaya ilitambue taifa la Palestina kabla hata ya makubaliano ya mwisho kati ya Israel na Palestina. Huku ikiwa haijawa sera rasmi, mapendekezo kama hayo yanaonekana kuishinikiza Israel kuwakubali zaidi Wapalestina. Kouchner na Moratinos wamepongeza jitihada za Marekani na kazi ya mjumbe wa Marekani katika Mashariki ya Kati George Mitchell, lakini wamesema ni lazima Ulaya sasa kuchukua jukumu kubwa katika mpango wa amani kwa lengo la kufanikisha suluhisho la haraka.
Mawaziri wa kigeni wa EU walaani mauaji ya Al-Mabhuh
Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wamelaani vikali matumizi ya pasi bandia za kusafiria za Ulaya zilizotumiwa na washukiwa wa mauaji ya kiongozi wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas, Mahmud al-Mabhuh huko Dubai. Kauli hiyo wameitoa katika mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji na kwamba wanalaani pia matumizi ya kadi za benki zinavyoibwa kutoka kwa raia wa nchi za umoja huo. Akizungumza na waandishi habari, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uhispania, Miguel Angel Moratinos ameelezea wasi wasi wao jinsi pasi hizo za Ulaya zinavyoweza kutumiwa kwa malengo ya aina tofauti. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Avigdor Lieberman amekutana na mawaziri hao wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, katika kuuhakikishia umoja huo kwamba Israel haina uhusiano wowote na matumizi ya pasi za kusafiria za Uingereza, Ireland, Ufaransa na Ujerumani katika mauaji ya kiongozi huyo wa Hamas mwezi uliopita. Hata hivyo mawaziri hao hawajalitaja wazi wazi shirika la kijasusi la Israel-Mossad, lakini ni wazi kwamba wanalihusisha shirika hilo na matumizi ya pasi hizo za kusafiria katika matukio ya awali.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed