1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Uingereza zatangaza ulazima wa kupima Corona

31 Desemba 2022

Uingereza na Ufaransa zimejiunga na mataifa mengine yakiwemo Uhispania na Korea Kusini yaliyotangaza ulazima wa vipimo vya Corona kwa wasafiri kutoka China bara.

Italien | Corona-Tests bei Einreise aus China
Picha: Maule Maurizio/IPA/ABACA/picture alliance

Shirika la Afya Duniani limekutana na maafisa wa China kwa mazungumzo jana Ijumaa kuhusu kuongezeka kwa maambukizo ya ugonjwa wa UVIKO-19, na kuwahimiza kutoa takwimu za uhakika ili nchi nyingine zichukue hatua za kuzuia kusambaa kwa Corona.

Mazungumzo hayo yamejiri baada ya mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kuitaka China kuwa wazi kuhusu hali ya maambukizo ya ugonjwa wa UVIKO-19 katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu duniani.

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limeeleza kuwa mkutano huo ulifanyika ili kutafuta kile ilichokiita "taarifa zaidi kuhusu hali ya maambukizo, na kutoa ushauri na usaidizi wa kitaalamu wa WHO."

Soma pia: China: Maandamano yaenea kupinga sera kali za kudhibiti UVIKO

Kuongezeka kwa maambukizo nchini China kumezua wasiwasi duniani kote na maswali kuhusu takwimu halisi za wagonjwa. Beijing imeorodesha idadi ndogo ya maambukizo na vifo kutokana na ugonjwa huo unaoshambulia zaidi mapafu licha ya hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti kulemewa.

Uingereza na Ufaransa zimejiunga na mataifa mengine ikiwemo Uhispania na Korea Kusini yaliyotangaza ulazima wa vipimo vya Corona kwa wasafiri kutoka China bara.

WHO: China inafaa kutoa takwimu kamili za wagonjwa wa UVIKO-19

Picha: Yonhap/picture alliance

Paris imeanzisha upimaji wa lazima kwa wasafiri kutoka China kuanzia Januari 1. Waziri wa afya wa Ufaransa Franois Braun amesema wasafiri kutoka China watahitajika kuonyesha kipimo cha PCR kisichozidi saa 48.

Kadhalika, wasafiri watalazimika kuvaa barakoa ndani ya ndege zinazoelekea Ufaransa na kipimo cha PCR kufanywa pindi wasafiri watakapowasili nchini humo. Waziri Braun ameeleza kuwa, sampuli za wagonjwa wa UVIKO-19 zitapelekwa kwa maabara kwa ajili ya uchunguzi.

Serikali ya Uingereza nayo imeweka sheria inayowalazimu wasafiri kutoka China kuonyesha kipimo cha Corona kuanzia Januari, 5.

Hatua kama hiyo pia imechukuliwa na Uhispania huku Waziri wake wa afya Carolina Darias akisema jana Ijumaa kuwa wasafiri kutoka China watalazimika kupimwa virusi vya Corona ama angalau mtu kuwa na dozi zote za chanjo dhidi ya UVIKO-19 kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Soma pia:Chanjo za Covid-19 zaathiri hedhi kwa kina mama

Darias hata hivyo hakuweza wazi tarehe kamili ambapo sheria hizo mpya zitaanza kutumika, akisema tu kwamba tangazo litatolewa hivi karibuni. Uhispania imeeleza kuwa, itajaribu kuwa na sheria ya pamoja kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala hili haraka iwezekanavyo.

Tayari nchi kadhaa zikiwemo Marekani na Italia zimeanzisha au kutangaza vikwazo vipya vya kuingia nchini humo. Jana Ijumaa, Korea Kusini ilisema kwamba kuanzia Jumatatu, wasafiri watatakiwa kuwasilisha vipimo vya PCR vya kuonyesha hawana maambukizo ya Corona baada ya kuwasili kutoka China.

Japan nayo ilitangaza kuwa itaanza sheria kama hizo, na kuwa safari za ndege za moja kwa moja kutoka China hadi katika viwanja vikuu vya ndege vya Japan pia zitapungua.

Umoja wa Ulaya watoa mwito kwa nchi za ukanda huo kuwa macho

Abiria wakipita karibu na bango la kuonyesha safari za ndege katika mji mkuu wa China, BeijingPicha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Umoja wa Ulaya unatafakari kuweka vikwazo zaidi. Baada ya kuandaa mkutano juu ya suala hilo mnamo siku ya Alhamisi, Kamishna wa afya wa Umoja huo Stella Kyriakides ametoa wito kwa nchi kuangazia upya ufuatiliaji wa wasafiri na aidha kuzidisha vikwazo iwapo kutakuwa na ulazima huo, akitahadharisha juu ya aina mpya ya virusi vya Corona.

Waziri wa afya wa Ujerumani Karl Lauterbach alisema jana Ijumaa kwamba upimaji wa lazima "bado hauhitajiki," japo viwanja vya ndege vya mataifa ya Ulaya vinatakiwa kuwa macho.

Soma pia: Kwa wajane Afrika, COVID-19 iliiba waume, nyumba, mustakablali

"Zaidi ya hapo, nadhani ni muhimu kwa mataifa ya Ulaya kuwa waangalifu juu ya suala hilo," Lauterbach alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kuwa, anaelewa kwanini baadhi ya mataifa yamechukua hatua ya kuweka ulazima wa vipimo vya Corona kwa sababu China "haijaweka wazi taarifa kamili" kuhusu mripuko wa hivi karibuni wa UVIKO-19.

China kwa sasa inapambana na ongezeko kubwa la maambukizo ya UVIKO-19. Katika wiki tatu za kwanza za mwezi Disemba pekee, watu milioni 248 walikutwa na virusi vya Corona, kulingana na makadirio ya ndani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW