Ujerumani, Ufaransa kuanzisha baraza la pamoja la usalama
7 Mei 2025
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Kansela huyo wa Ujerumani tangu alipoingia mamlakani Jumanne 06.05.2025. Nchi hizo mbili zimefanya makubaliano hayo ya kuunda baraza la usalama litakalokutana mara kwa mara kama sehemu ya juhudi za kuongeza uwekezaji katika ulinzi. Makubaliano hayo yamefikiwa huku Ulaya ikifanya juhudi za kuimarisha ulinzi wakati Ukraine ikikabiliwa na vita dhidi ya Urusi.
Soma zaidi: Friedrich Merz afanya ziara yake ya kwanza Ufaransa na Ujerumani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amefafanua zaidi kuhusu makubaliano hayo na kusema, "Tutaharakisha programu zetu za Ujerumani na Ufaransa na kuimarisha uwezo wetu. Mbali na mizinga, ndege za kivita na makombora ya masafa marefu, tutaanzisha baraza la usalama litakalotoa majibu ya kiutendaji kwa changamoto zetu za kimkakati."
Zaidi Macron ameeleza kuwa nchi hizo mbili zinataka kufanya kazi pamoja katika mambo zinayoyapa kipaumbele yakiwemo uhuru, ulinzi na ushindani huku akisisitiza kuwa jukumu kubwa kabisa la Ufaransa na Ujerumani ni kudumisha ulinzi barani Ulaya.
Ushirikiano kuelekezwa pia kwenye uchumi, na fedha
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema nchi yake na Ufaransa zitaongeza pia ushirikiano katika maeneo mengine kadhaa. Merz ameeleza kuwa, "Ninataka kuweka wazi kuwa serikali zetu zinachukua majukumu ya pamoja, yakiwemo katika kazi ambayo tayari inafanyika kwenye wizara tofauti. Tutaongeza juhudi katika maeneo yote kama vile katika sera ya uchumi, kwenye sera ya usalama, ulinzi na ya fedha ili kuziimarisha"
Ameyasema hayo akiwa sambamba na Rais Macron na kuongeza kuwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya zinapaswa kuongeza bajeti zao za ulinzi ili kuziba mwanya katika uwezo wa jumuiya hiyo na kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Soma zaidi: Merz afanya ziara ya kushtukiza Paris kwa mazungumzo na Macron
Baada ya kukutana na Macron, Merz anaelekea nchini Poland atakapokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Donald Tusk.
Ameanza siku yake ya kwanza kazini kwa kufanya ziara katika mataifa hayo mawili wakati Ulaya ikifanya jitihada za kuongeza uwezo wake wa kujilinda kukiwa pia na mashaka kuhusu dhamira ya Marekani kwa usalama wa Ulaya. Hata hivyo ameseisitiza kuwa makubaliano yoyote ya amani ya Ukraine yanahitaji Marekani ishirikishwe.