Ufaransa na Ujerumani zasisitiza ushirikiano wao
24 Juni 2017Viongozi hao wawili wa Ujerumani na Ufaransa walikuwa na mkutano usio wa kawaida wa pamoja na waandishi habari baada ya kukutana na wenzao 26 wa Umoja wa Ulaya.
"Wakati Ujerumani na Ufaransa zikizungumza kwa sauti moja, Ulaya inaweza kusongambele," rais mpya Macron aliwaambia waandishi habari waliojazana katika chumba cha mkutano wakati akisimama pamoja na kansela wa Ujerumani.
"Hakutakuwa na suluhisho la mfungamano iwapo sio suluhisho la mfungamano kwa Ufaransa na Ujerumani," kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 39 anayefuata siasa za wastani za mrengo wa kati alisema.
Licha ya mtazamo wake wa nadharia za vitendo zaidi , ujumbe kutoka kwa Merkel mwenye umri wa miaka 62 ulikuwa huo huo.
"Mkutano huu na waandishi habari unaonesha kwamba tumeamua kujiunga pamoja kutafuta suluhisho kwa ajili ya matatizo," amesema Merkel.
Mkutano huo wa pamoja na waandishi habari umekuja mwaka mmoja kamili baada ya kura ya kushitua ya maoni kwa Uingereza kuwa nchi ya kwanza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya , hali iliyosababisha utabiri wa kuvunjika kwa Umoja huo.
Ulaya yaweka kando siasa kali
Lakini Ulaya imepanda katika mkokoteni wa ushindi wa kushitua wa Macron dhidi ya kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa Marine Le Pen na kupuliza tarumbeta la matumaini baada ya miaka ya kubana matumizi na mzozo licha ya kujitoa kwa Uingereza, Brexit.
Katikati ya hilo kuna wazo kwamba macron huenda atafanikiwa kuufanyia ukarabati "moyo" wa utamaduni nyuma ya ujumuisho wa Ulaya , ushirikiano wa baada ya vita wa Ufaransa na Ujerumani baada ya karne kadhaa za mizozo.
Viongozi wa Ufaransa na Ujerumani , wengi wakiuita kwa jina la utani Merkron , Mackerel na Emmangela ni mtindo wa majina ya utani ya watu hao maarufu, kusema wanania ya kutumia nguvu hizo kusonga mbele.
Macron amesisitiza kuhusu umoja wao katika masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa bara la Ulaya , wakati bara hilo likishindwa kuzitegemea Uingereza ama Marekani chini ya Donald Trump.
Baada ya Marekani kuitupa mkono Ulaya
Pia wametangaza kuwapo kwao pamoja kuhusiana na suala la mabadiliko ya tabianchi, hususan baada ya Trump kujitoa kutoka mkataba wa Paris wa mazingira, mapambano dhidi ya ugaidi na masuala ya biashara.
Hata hivyo walikuwa waangalifu kwa kukwepa kuingia ndani zaidi kutoa maelezo katika masuala nyeti kama mageuzi ya kanda ya euro, mradi maalum wa Macron ambaye anataka nchi hizo ziwe na bunge lake lenyewe pamoja na waziri wa fedha.
"Hatutangazi mapema mambo ambayo hatuwezi kuyaendeleza," alisema kansela Merkel ambaye mara nyingi ni mtu anayesema jambo la maana, wakati alipoulizwa iwapo hatimaye wataamua kutumia mapendekezo kamili baada ya uchaguzi wa Ujerumani mwezi Septemba.
Viongozi hao wawili pia walichukua msimamo wa tahadhari kuelekea waziri pendekezo la waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuhusiana na haki ya raia wa Umoja wa Ulaya wanaoishi nchini Uingereza baada ya mchakato wa Brexit.
Lakini katika eneo moja, Macron huenda aligundua kwamba fungate ya mkutano huo ilikuwa imekwisha kabla ya kuanza.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra Buwayhid