Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kuendeleza vikwazo kwa Iran
15 Septemba 2023Vikwazo hivyo vilitarajiwa kumalizika muda wake mwezi Oktoba mwaka huu, kulingana na ratiba iliyoainishwa katika mkataba uliovunjika kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Katika taarifa ya pamoja, mataifa hayo matatu washirika ya barani Ulaya yamesema kuwa yataendelea kuiwekea vikwazo Iran ikiwa ni majibu kwa nchi hiyo ambayo imeshindwa kuuheshimu mkataba huo.
Soma zaidi: Ulaya yakiri kupokea majibu ya Iran kuhusu mkataba wa nyuklia
Vikwazo iliyowekewa Iran kutokana na ukiukwaji wa makubaliano hayo ni pamoja na kuipiga marufuku kuzalisha silaha za nyuklia na kumzuia mtu yeyote kununua, kuuza au kusafirisha ndege zisizo na rubani kutoka au kwenda Iran.
Hatua nyingine ni pamoja na kuzizuia mali za raia kadhaa wa Iran na wale wanaohusika katika mpango wa nyuklia na programu ya utengenezaji wa makombora ya masafa marefu. Iran imekiuka vikwazo hivyo kwa kuzalisha na kufanya majaribio ya makombora hayo na kupeleka ndege zisizo na rubani nchini Urusi kwa ajili ya vita dhidi ya Ukraine.
Taarifa ya pamoja ya Uingereza, Ujerumani na Ufaransa imeeleza kuwa, vikwazo vitaendelea hadi pale Iran itakapoyaheshimu makubaliano hayo.
Iran yalaani kuendelea kuwekewa vikwazo
Kutokana na hatua hiyo, wizara ya mambo ya kigeni ya Iran kupitia shirika rasmi la habari la Iran IRNA, imeuita uamuzi wa mataifa hayo kuwa ni kinyume cha sheria na ya kichokozi, na kwamba yatarudisha nyuma ushirikiano.
Wizara hiyo imeongeza kuwa vitendo vya washirika hao wa Ulaya kwa hakika vitakuwa na madhara katika juhudi za kukabiliana na mivutano.
Mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 ulisainiwa ili kuhakikisha kuwa Iran haitengenezi silaha za nyuklia. Chini ya makubaliano hayo Tehran ilikubali kupunguza urutubishaji wa madini ya Urani ili iondolewe vikwazo vya kiuchumi.
Mwaka 2018, aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo Donald Trump aliiondoa nchi yake kwenye mkataba huo akisema kuwa angefanya mazungumzo kwa ajili ya kupata mkataba mzuri zaidi, lakini hilo halikutokea.
Soma zaidi: Mkuu wa IAEA aridhishwa mazungumzo na Iran
Iran ilianza kuyakiuka makubaliano mwaka mmoja baadaye na sasa inarutubisha madini ya Urani kwa viwango vinavyotosha kutengeneza silaha, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia nyuklia. Mazungumzo yaliyokuwa na nia ya kutafuta mwongozo wa kurejea tena kwenye mkataba huo, yalivunjika mwezi Agosti mwaka 2022.
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeshamuarifu Mkuu wa Sera za Umoja wa Ulaya Josep Borell aliyesema ameipeleka barua yao kwa kwa nchi zilizotia sahihi mkataba huo mwaka 2015 ambazo ni China, Urusi na Iran