1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yafanya uchaguzi wa rais

10 Aprili 2022

Vituo vya kupigia kura nchini Ufaransa vitafungwa jioni hii baada ya uchaguzi wa rais ambao rais wa sasa Emmanuel Macron anawania muhula wa pili. Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa usiku wa leo Jumapili.

Frankreich | Präsidentschaftswahlen | Wahllokal in Le Touquet
Picha: AFP via Getty Images

Kulingana na kura za maoni ya umma ni wazi kutakuwa na duru ya pili kati ya Macron na mpinzani wake wa karibu mwanasiasa wa mrengo wa mkali wa kulia  Marine Le Pen.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema asubuhi ya Jumapili baada ya kampeni ya uchaguzi isiyo ya kawaida iliyotiwa kiwingu na vita nchini Ukraine. Wachambuzi wamekwishakuonya suala la uvamizi huo wa Urusi unaweza kubadili matarajio ya matokeo ya uchaguzi wa Ufaransa.

Ishara za mwanzo zinaonesha idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni pungufu kwa asilimia 3 ya wale waliteremka vituoni mnamo mwaka 2017.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Briggette wakielekea kupiga kura Picha: Thibault Camus/Pool/AP/picture alliance

Maoni ya umma yanatabiri Macron atampiku Le Pen kwa asilimi ndogo katika duru hii ya kwanza na wawili hao ndiyo watachuana kwenye duru ya pili mnamo Aprili 24.

Mgombea wa mrengo mkali wa kushoto Jean-Luc Melenchon ndiye anayejikongoja nyuma ya wawili hao akiwa yungali na matumaini ya kuruka vigingi vya kuingia duru ya pili iwapo matokeo yanawaendea kombo Macron au Bibi Le Pen.

Macron na mkewe wapiga kura upande wa kaskazini 

Mgombea wa urais nchini Ufaransa Marine Le Pen Picha: Denis Charlet/AFP/Getty Images

Rais Macron akifuatana na mkewe Brigitte alipiga kura yake katika kitongoji cha Le Touquet kaskazini mwa mwambao wa bahari ya Ufaransa. Le Pen alikwenda kupiga kura upande huo huo wa kaskazini lakini mji mdogo wa Henin-Beaumont na Melenchon alipiga kura yake katika mji wa bandari wa kusini mwa Ufaransa wa Marseille.

Ingawa wapinzani wake wanamkosoa kwa mwanasiasa mwenye misimamo mikali, Le Pen alichagua kuonesha taswira ya tofauti kwenye kampeni za mwaka huu kwa kuchukua msimamo wa wastani kuhusu masuala tete kama uhamiaji na ushawishi wa dini ya kiislamu kwenye taifa hilo lenye ushawishi barani Ulaya.

Pia kampeni yake ilituama juu ya masuala yanayowatatiza Wafaransa wengi hususani kupanga kwa bei za bidhaa, nishati na vyakula.

Macron kwa upande wake alifanya kampeni kwa muda mfupi sana. Hivi karibuni alikaririwa akijilaumu mwenyewe kwamba alitamani angelianza kampeni yake mapema lakini ilishindikana kutokana na mzozo unaoikabili Ukraine.

Baada ya vituo kufungwa saa kumi na mbili jioni, vituo vya televisheni nchini Ufaransa vitaanza kutoa matokeo ya awali.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW