1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yagoma kuchunguza upya kifo cha Habyarimana.

3 Julai 2020

Mahakama ya rufaa ya nchini Ufaransa imekataa ombi la kufungua upya uchunguzi kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa rais wa Rwanda, mnamo mwaka 1994, Juvenal Habyarimana, ambayo yalichochea mauaji ya kimbari ya watu 800,000.

Juvenal Habyarimana 1990
Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa hiyo ilitolewa na mawakili.

Kulingana na mawakili wa familia za wale waliouawa pamoja na Habyarimana wakati ndege yake ilipodunguliwa, wanatarajia kukatia rufaa uamuzi huo wa mahakama ya Ufaransa.

Mahakama hiyo ya rufaa ya Ufaransa, iliombwa kupitia upya uamuziuliotolewa mwaka 2018 wa kuachana na uchunguzi dhidi ya waliokuwa washirika tisa na wengine wa zamani wa rais Paul Kagame, katika kesi ambayo ilitia doa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira wa kabila ya Hutu pia aliuawa

Ndege iliyokuwa imembeba rais Juvenal Habyarimana aliyetokea jamii ya Wahutu, ilidunguliwa mjini Kigali Aprili 6, 1994, hatua iliyoibua mauaji ya kimbari ya watu 800,000, hususan kutoka kabila ya Tutsi, lakini pia Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani waliuawa.

Rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira wa kabila ya Hutu pia aliuawa kufuatia shambulizi hilo la ndege hiyo iliyodunguliwa na angalau kombora moja wakati ilipokuwa njia kuelekea kutua mjini Kigali.

Jeneza la rais wa zamani wa Burundi Cyprien NtaryamiraPicha: P.Guyot/AFP/GettyImages

Uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ulianzishwa nchini Ufaransa mnamo mwaka 1998, kufuatia malalamiko ya familia za wafanyakazi wa ndege hiyo ya Ufaransa.

Uchunguzi huo, awali uliwaangazia zaidi washirika wa rais Kagame, Mtutsi aliyeongoza vuguvugu la waasi wa Rwandan Patriotic Front, RPF na hatimaye kuingia mamlakani baada ya kuuangusha utawala wa Kihutu.

Kagame, ambaye ni rais wa Rwanda tangu mwaka 2000, alivunja mahusiano ya kidiplomasia na Ufaransa kati ya mwaka 2006 na 2009 baada ya Ufaransa kutoa waranti wa kukamatwa washirika wake.

Na mnamo mwaka 2012, ripoti iliyochapishwa na wataalamu kutoka Ufaransa, ilisema kombora hilo lilifyatuliwa kutoka kwenye kambi ya Kanombe iliyokuwa ikidhibitiwa na jeshi la Habyarimana, na kubadilisha mkondo wa uchunguzi.

Kagame aliituhumu Ufaransa katika maadhimisho ya miaka 20 ya mauaji ya Kimbari

Kigali ilisema kwamba uchunguzi huo ulithibitisha imani yake kwamba shambulizi hilo lilifanywa na Wahutu wenye itikadi kali walioamini kwamba Habyarimana alikuwa na misimamo ya wastani mno na aliyepinga mchakato wa amani wa Arusha uliokuwa ukiendelea wakati huo.

Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: Presidence RDC

Wakati uchunguzi ukiwa bado unaendelea taratibu, Kagame aliituhumu Ufaransa katika maadhimisho ya miaka 20 ya mauaji ya Kimbari mwaka 2014 kwa kuwa na jukumu la moja kwa moja kwenye mauaji hayo. Na mwezi Novemba ilianzisha uchunguzi dhidi ya madai ya maafisa wa Ufaransa kuhusika na mauaji ya kimbari.

Ufaransa hata hivyo inakana madai hayo na mwaka jana, rais Emmanuel Macron alitangaza kuundwa kwa jopo la wanahistoria na watafiti kuchunguza madai hayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW