1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yahimiza umoja katika mazungumzo na Uingereza

Daniel Gakuba
13 Oktoba 2020

Ufaransa imehimiza umoja miongoni mwa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, katika mazungumzo na Uingereza, hususan kuhusu haki za uvuvi mojawapo ya kipengele kigumu katika mazungumzo hayo juu ya uhusiano wa baadaye

Symbolbild Brexit Verhandlungen
Picha: picture-alliance/empics/S. Rousseau

Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya Ulaya Clement Beaune, akizungumza na mawaziri wenzake kutoka nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya, amesema kuna umuhimu wa nchi zote za umoja huo kuendelea kuwa na msimamo mmoja, katika mazungumzo kuhusu uhusiano wa baadaye na Uingereza, maarufu kama Brexit.

Waziri Beaune amesema lazima umoja huo usitetereke katika kutetea vipaumbele vyake, kama haki ya uvuvi na vigezo sawa vya ushindani, ambavyo kwa maoni yake ni lazima kukubaliwa kabla ya Uingereza kupata ruhusa ya kulifikia bila vizuizi soko la Umoja wa Ulaya wenye wakaazi milioni 450.

Uingereza, ambayo uanachama wake katika Umoja wa Ulaya ulimalizika rasmi mwishoni mwishoni mwa mwaka jana, inaendelea kushiriki katika soko la pamoja la umoja huo kwa mwaka mmoja zaidi, hadi mwishoni mwa Desemba mwaka huu. Mazungumzo yanayoendelea yananuia kuendeleza ushirikiano huo hata baada ya muda huo.

Waziri wa Ufaransa kuhusu mambo ya Ulaya Clement Beaune Picha: Petros Karadjias/AP Photo/picture-alliance

Kama Ufaransa, Ujerumani inaitaka Uingereza kujitolea zaidi katika majadiliano yanayohusu haki za uvuvi, na ruzuku za serikali kwa makampuni yake, ikisema mazungumzo hayo yamefika katika wakati hatua nyeti kabisa.

Waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex, akizungumza mapema wiki hii, alisema ingawa nchi yake ingependa yawe makubaliano ya ushirikiano wa baadaye na Uingereza baada ya nchi hiyo kuondoka kikamilifu katika Umoja wa Ulaya, nchi yake, kwa ushirikiano wa karibu na washirika wengine wa Ulaya, ilikuwa tayari kwa chochote kitakachotokea.

Uingereza pia imeelezea msimamo kama huo. Waziri wake mkuu Boris Johnson alizungumza na rais waUfaransa Emmanuel Macron mwishoni mwa Juma lililopita, na kuweka Alhamis ya wiki kama siku ya mwisho anayotaka kufahamu ikiwa makubaliano ya Brexit yatafanikiwa au yatagonga mwamba.

Ikiwa mazungumzo hayo yatashindikana, mtiririko wa biashara kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya utasitishwa tarehe mosi Januari mwaka ujao, na vizuizi vya mpakani vitaanza kutumiwa, hali inayohofiwa itachelewesha usafirishaji wa bidhaa, na kusababisha mlundikano wa malori katika vituo vya ukaguzi.

dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW