1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaiunga mkono Ukraine mpango wa kukomesha vita

19 Oktoba 2024

Ufaransa inasema inauunga mkono mpango wa Ukraine wa kuvimaliza vita vya miaka miwili na nusu kufuatia uvamizi wa Urusi wa Februari 2022.

Jean-Noel Barrot
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot.Picha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, aliwaambia waandishi wa habari mjini Kiev siku ya Jumamosi (Oktoba 19) kwamba angelishirikiana na maafisa wa Ukraine kupata uungaji mkono wa mataifa mengine kwa mpango huo wa amani ya kudumu.

Mpango huo uliozinduliwa na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwa jina la "mpango wa ushindi" unalenga kuilazimisha Urusi kukomesha uvamizi wake kupitia majadiliano.

Soma zaidi: Zelensky adai Korea Kaskazini yaandaliwa kwa vita

Mpango huo unatathminiwa hivi sasa na washirika wa Ukraine wa mataifa ya Magharibi, ambao msaada wao ni muhimu sana kwa Kiev kuweza kupambana na Urusi - jirani mkubwa mwenye nguvu nyingi za kijeshi. 

Sehemu muhimu kwenye mpango huo ni kuialika Ukraine kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa NATO, uamuzi ambao mataifa ya Magharibi yamekuwa yakijizuwia kuuchukuwa kabla ya kumalizika kwa vita hivyo.

"Ushindi wa Urusi utakuwa ni kuhalalisha sheria ya porini ya mwenye nguvu ndiye mwenye haki na kuuingiza mfumo wa kimataifa kwenye machafuko makubwa," Barrot alisema kwenye mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari kati yake na mwenzake wa Ukraine, Andrii Sybiha.

"Ndio maana majadiliano yetu lazima yatuwezeshe kupiga hatua kuelekea kwenye mpango wa ushindi wa Rais Zelensky na kuzishawishi nchi nyengine nyingi kadiri iwezekanavyo kuunga mkono." Aliongeza Barrot.

Msaada wa Ufaransa kwa Ukraine

Waziri huyo wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa alisema nchi yake itaikabidhi Ukraine sehemu ya mwanzo ya msaada wa ndege za kijeshi ndani ya kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka 2025. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Adrii Sybiha (kulia), akimkaribisha mwenzake wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, mjini Kiev siku ya Jumamosi (Oktoba 19, 2024).Picha: Alex Babenko/AP/picture alliance

Ufaransa pia itatowa mafunzo kwa marubani ili waweze kuziendesha wenyewe na mafundi wa ndege ili waweze kuzitengeneza wenyewe.

Soma zaidi: Zelensky awasilisha Mpango wa Amani wakati ikijiandaa na Mkutano ujao wa Amani

Tangu mwaka 2022, Ufaransa imekuwa mmojawapo wa waungaji mkono wakubwa wa Ukraine sio tu kijeshi, bali pia kidiplomasia na kiuchumi barani Ulaya. Hivi sasa inaendelea kuwapa mafunzo na vifaa wanajeshi wa Ukraine kuunda kile kinachoitwa brigedia ya kwanza kamili na mpya kwenye mstari wa mbele wa mapigano.

"Kwa kupambana dhidi ya mvamizi kwa ujasiri usio mfano, sio tu munapigania heshima ya mamlaka ya Ukraine, lakini munaongoza mstari wa mbele wa mapambao unaoitenganisha Ulaya na Urusi ya Vladimir Putin, unaotenganisha uhuru na ukandamizaji." Alisema Barrot mjini Kiev.

Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa wa kivita

Ziara ya Barrot mjini Kiev ilisadifiana na tukio la mabadilishano ya wafungwa wa kivita kati ya Urusi na Ukraine usiku wa Ijumaa (18 Oktoba), ambayo yalihusisha wafungwa 190 kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Falme wa Kiarabu.

Wafungwa wa kivita wa Ukraine wakikaribishwa nyumbani baada ya mabadilishano ya wafungwa kati ya nchi yao na Urusi.Picha: Ukraine's President Volodymyr Zelenskiy Via Telegram/Handout/REUTERS

Miongoni mwa wafungwa 95 wa Ukraine, walikuwamo wapiganaji 34 wa Azov waliokuwa wakiulinda mji wa Mariupol na kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mapigano yaliyotajwa kuwa makali na ya aina yake katika miaka miwili na nusu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

"Watu wetu 95 wamerudi nyumbani. Hawa ni mashujaa walioitetea Mariupol na 'Azovstal', na pia Donetsk, Luhansk, Kharkiv, Kiev, Cherniv na Kherson," aliandika Zelensky kwenye ujumbe wake katika mtandao wa X.

Soma zaidi: Urusi yaongeza shinikizo kwa kushambulia zaidi Donestk

Mkuu wa kikosi cha Azov, Denys Prokopenko, alisema kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba wapiganaji 34 wa Azov walikuwa wamerejeshwa, lakini wengine 900 bado wako kwenye mikono ya Urusi.

Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binaadamu nchini Ukraine, Maksym Butkevych, alikuwa mmoja wa wafungwa 95 waliokuwamo kwenye mpango huo wa mabadilishano. Kuachiliwa kwake kulitangazwa na Kituo cha Haki za Binaadamu cha ZMA, ambacho yeye ni mwanzilishi mwenza.

Mabadilishano hayo yalifuatiwa na kurejeshwa kwa miili 501 ya wanajeshi wa Ukraine siku ya Ijumaa katika kile kilichoonekana kama idadi kubwa zaidi ya maiti za wanajeshi kurejeshwa kwa wakati mmoja tangu uvamizi wa Urusi uanze mnamo Februari 2022.

Wengi wa wanajeshi hao waliuawa wakiwa kwenye mapambano mashariki mwa mkoa wa Donetsk, hasa kuzunguka mji wa Avdiivka ambao vikosi vya Urusi viliutwaa mwezi Februari baada ya mapigano makali, kwa mujibu wa Idara ya Uratibu wa Wafungwa wa Kivita ya Ukraine.

Kwa upande wake, Urusi ilipokea miili 89 ya wanajeshi wake, kwa mujibu wa mbunge Shamsayil Saraliyev.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW