Wafaransa waandamana kupinga hatua za rais Macron
10 Septemba 2025
Sébastien Lecornu , aliyechaguliwa na Rais Emmanuel Macron kuwa waziri mkuu wa tano wa Ufaransa katika kipindi cha miaka miwili, alikabidhiwa ofisi ya Matignon na Waziri Mkuu anaeondoka Francois Bayrou, ambaye serikali yake iliangushwa baada ya kushindwa kura ya imani Bungeni.
Lecornu mwenye umri wa miaka 39, ambaye alikuwa waziri wa ulinzi na mwanasiasa mtiifu kwa Macron , amechukua usukani wakati maandamano yakiongozwa na kikundi cha mrengo wa kushoto yakishuhudiwa sehemu mbalimbali huko Ufaransa chini ya kauli mbiu ya "kuzuia kila kitu".
Maandamano hayo yameshuhudiwa katika miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na mji mkuu Paris, Lyon, Bordeaux, Marseille na kwengineko. Takriban maafisa wa polisi 80,000 wamesambazwa kote Ufaransa huku waandamanaji wakiweka vizuizi kwa kutumia mapipa ya taka, mabango na hivyo kuzuia barabara na kuvuruga huduma muhimu kama usafiri na shule.
Waandamanaji zaidi ya 200 wakamatwa
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa anayeondoka Bruno Retailleau amesema maandamano ya vurugu hayatovumiliwa na kutangaza kuwa tayari watu karibu 250 wamekamatwa. Waandamanaji wanapinga vikali uamuzi wa Macron wa kumteua mshirika wake wa karibu kuwa waziri mkuu wakilalamika kuwa wanahitaji mabadiliko.
Macron alimteua Lecornu jana jioni, siku moja baada ya mtangulizi wake Francois Bayrou kupoteza kura ya imani yake bungeni kufuatia jaribio lake la kutaka kupitisha bajeti iliyopingwa vikali na wabunge na ambayo ilijikita zaidi katika kubana matumizi hadi dola bilioni 52 ili kupunguza deni la Ufaransa.
Lecornu aahidi kuja na sera mpya
Lecornu anayekuwa waziri mkuu wa saba tangu Macron aingie madarakani mwaka 2017 na wa tatu ndani ya muda wa mwaka mmoja pekee amesema atalihutubia taifa katika siku zijazo ili kuelezea sera zake, akiahidi kuwa zitakuwa na utofauti mkubwa na zile zilizopita:
" Kimsingi tunapaswa kukomesha hali hii ya kutozingatia uhalisia: Hasa huu wa utofauti kati ya hali ya kisiasa na kile ambacho raia wenzetu wanachokitarajia katika maisha yao ya kila siku, uhalisia wa hali ya kiuchumi na kijamii na kwa usalama wao. Kwa ufupi, hili ndilo jukumu kuu tulilopewa."
Maandamano haya mapya yaliyoibuka sehemu mbalimbali nchini Ufaransa, yanakumbushia vuguvugu dhidi ya serikali lililofahamika zaidi kwa kifaransa kama "Gilets-Jaune" yaani vizibao vya Njano ambalo liliibuka mwaka 2018 bila ya kuwa na uongozi ulio wazi lakini lililoibua changamoto kubwa kwa Macron wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani.
// AFP, DPA, AP