1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Ufaransa: Maalfu wapinga mageuzi ya umri wa kustaafu

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
20 Januari 2023

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12, vyama vya wafanyakazi nchini Ufaransa vimeandaa maandamno makubwa ya kupinga mageuzi ya umri wa kustaafu ambao serikali inataka kuuongeza kutoka miaka 62 hadi miaka 64.

Frankreich I Landesweiter Streik gegen die Rentenreform
Picha: Bart Biesemans/REUTERS

Zaidi ya watu milioni moja wameandamana nchini Ufaransa kupinga mageuzi katika mfumo wa pensheni, huku baadhi ya waandamanaji wakikabiliana na polisi mjini Paris. Mgomo huo ulivuruga shughuli za usafiri wa umma hapo siku ya Alhamis, vilevile shule na sehemu kubwa ya shughuli za utumishi wa umma ziliathirika pia.

Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imesema, nchini kote jumla ya wanaoandamana kupinga mpango wa Rais Emmanuel Macron wa kuongeza umri wa kustaafu ni watu milioni 1.2, miongoni mwao watu 80,000 katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris. Muungano wa vyama vya mrengo mkali wa kushoto CGT kwa upande wao wamesema zaidi ya watu milioni mbili wameshiriki kwenye maandamano hayo kote nchini Ufaransa, na katika mji mkuu Paris walijitokeza watu 400,000. Muungano huo wa vyama vya mrengo wa kushoto umesema maandamano mengine yamepangwa kufanyika Januari 31.

Mfanyakazi wa shirika la reli amebeba bendera ya muungano wa vyama vya mrengo mkali wa kushoto CGT akipinga mpango wa kuongeza umri wa kustaafu.Picha: Stephane Mahe/REUTERS

Jioni ya jana kwenye maandamano hayo imeripotiwa kwamba kulikuweko makundi ya waandamanaji vijana waliopambana na vikosi vya usalama mashariki mwa jiji la Paris, ambapo baiskeli kadhaazilichomwa moto na baadhi ya vituo vya mabasi viliharibiwa.

Polisi imesema watu 44 walikamatwa kwa makosa ya kuwa na silaha au kufanya ghasia, wengi wao ni wafuasi wa kundi la itikadi kali linaloitwa "Black Blocs". Mpango wa pensheni, uliowasilishwa na serikali ya Macron wiki iliyopita, unalenga kuongeza umri wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi miaka 64 jambo ambalo wengi wanalipinga.

Waandamanji waupinga mpango wa serikali ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wa mageuzi katika utaratibu wa pensheni.Picha: Benoit Tessier/REUTERS

Hata hivyo waziri wa fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire ameiambia televisheni ya Bloomberg kwenye  Kongmano la Uchumi Duniani mjini Davos  leo Ijumaa kwamba migomo iliyoanza hivi majuzi ya kupinga mipango ya serikali ya Ufaransa ya kuongeza umri wa kustaafu haiwezi kuathiri hata chembe uchumi wa nchi.  Le Maire aliongeza kusema kuwa uchumi wa Ufaransa uko imara na unaendelea vizuri.

Vyanzo: AFP/RTRE

 

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW