Ufaransa yalaumu ulaghai wa tiketi kwa vurugu za fainali
30 Mei 2022Vurugu hizo ziliibua maswali kuhusu uwezo wa Paris kuandaa Michezo ya Olimpiki ya 2024. Serikali ya Ufaransa imekabiliwa na shutuma nyingi kutoka kwa vyombo vya habari na wanasiasa nchini Uingereza kwa namna polisi ilivyoisimamia mechi hiyo ya Jumamosi, ambapo maelfu ya mashabiki wa Liverpool waliokuwa na tiketi walikumbwa na changamoto kuingia dimba la Stade de France.
Baada ya mkutano wa dharura leo katika wizara ya michezo, Waziri wa Usalama wa Ndani Gerald Darmanin alisisitiza waziwazi kuwa ulaghai wa tiketi na fujo za mashabiki wa Liverpool ndivyo vinapaswa kulaumiwa. "Kilichogundulika ni ulaghai mkubwa na wa kupangwa wa tiketi bandia kwa sababu ukaguzi uliofanywa na walinzi wa uwanjani, dimba la Stade de France na shirikisho la kandanda la Ufaransa ulitabiri zaidi ya asilimia 70 ya tiketi bandia katika lango kuu. Kisha, baada ya ukaguzi wa awali kukamilika, ikagundulika kuwa zaidi ya asilimia 15 ya tiketi hizo zilikuwa bandia. Hii ni kumaanisha, kulikuwa na zaidi ya tiketi 2,600, idadi iliyothibitishwa na UEFA, ambazo hazikuidhinishwa hata ingawa zilikuwa zimepita ukaguzi wa awali."
Waziri wa Michezo Amelie Oudea-Castera amesema Ufaransa inawaomba radhi karibu mashabiki 2,700 ambao walikuwa na tiketi na hawakuweza kuingia dimbani kwa sababu ya matatizo ya kuudhibiti umati na kudokeza kuwa wafidiwe. "Kulikuwa na matazizo katika jinsi tulivyoshughulikia mmiminiko wa mashabiki. Hatutaki kusema kuwa tulifanya kila kitu sawa. Hapana. Lakini tunasema kulikuwa na sababu kadhaa zilizofanya mambo kuwa magumu. Mgomo katika vyombo vya usafiri, mashabiki kuchelewa kuwasili. Hakukuwa na safari ya wazi ya kutoka eneo la mashabiki waliokuwa mjini kwenda uwanjani. Kwa upande huo, ilikuwa tofauti sana na jinsi Real Madrid ilipanga kwa ajili ya mashabiki wao."
Mkutano wa leo ulilihusisha shirikisho la kandanda Ulaya – UEFA, wakuu wa kandanda la Ufaransa na polisi ya Ufaransa. Mkuu wa polisi mjini Paris Didier Lallement ametoa wito wa uchunguzi rasmi kuhusu utengezaji wa tiketi bandia ambazo alisema zilisaidia kuleta matatizo hayo. Ametetea kazi ya polisi akisema maafisa walizuia vifo ambavyo vingetokea kutokana na mkanyagano wa mashabiki nje ya uwanja. Watu 100 wamekamatwa kutokana na vurugu hizo.
afp