Ufaransa yamhukumu Claude Muhayimana miaka 14 jela
28 Februari 2026
Muhayimana mwenye umri wa miaka 65 zamani alikuwa akifanya kazi kama dereva katika hoteli moja huko Kibuye, kwenye kingo za Ziwa Kivu, magharibi mwa Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ambapo watu 800,000 waliuawa wengi wao wakiwa ni Watutsi. Dereva huyo wa zamani pia amepatikana na makosa ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinaadamu na kushiriki katika mauaji hayo ya kimbari.
Mahakama ya mjini Paris iligundua kuwa Muhayimana aliwasafirisha wanamgambo wa Interahamwe hadi kwenye maeneo ya Kibuye na vitongoji vyake ambapo makumi ya maelfu ya watu waliuawa. Claude Muhayimana aliikimbia Rwanda miezi michache baada ya mauaji hayo, akawasili Ufaransa mwaka wa 2001 na kupewa uraia wa Ufaransa mnamno mwaka 2010.
Mawakili wa Muhayimana Reda Ghilaci na Hugo Latrabe wamekosoa uamuzi huo kutokana na baadhi ya ushahidi kubadilishwa huku wakisema kuwa watakata rufaa ambayo kwa kawaida itakuwa ndio ya mwisho.