Ufaransa yapeleka wanajeshi zaidi Mali
15 Januari 2013Wakati huo huo, rais wa Ufaransa, Francois Hollande, yuko katika ziara ya siku moja katika Umoja wa Falme za Kiarabu akiyataka mataifa ya Kiarabu kusaidia katika juhudi za kupambana na waasi wa Kiislamu nchini Mali.
Ufaransa tayari imekwishapeleka mamia ya wanajeshi wake nchini Mali na inatarajia kutuma wanajeshi zaidi baada ya kufanya mashambulizi ya anga kwa siku kadhaa tangu Ijumaa iliyopita katika eneo kubwa la jangwa lililokamatwa mwaka jana na muungano wa makundi ya Kiislamu ambayo yanajumuisha pia tawi la kundi la al-Qaeda katika mataifa ya Afrika kaskazini pamoja na kundi la MUJWA linalotokea nchini Mali, pamoja na kundi la Ansar Dine.
Akizungumza kutoka katika kituo cha kijeshi cha Ufaransa mjini Abu Dhabi mwanzoni mwa ziara yake ya siku moja katika Umoja wa falme za Kiarabu, rais Francois Hollande amesema majeshi ya Ufaransa nchini Mali yamefanya mashambulio zaidi usiku wa jana, ambayo yamefanikiwa kushambulia mahali palipokusudiwa.
Ufaransa inakusudia kuweka jumla ya wanajeshi 2,500 katika koloni lake hilo la zamani kuimarisha jeshi la Mali pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na jeshi linaloingilia kati, lililotolewa na mataifa ya Afrika magharibi ya jumuiya ya ECOWAS.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa anayeongozana na rais na Hollande katika ziara hiyo ambayo ina lengo la kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuwezesha kupiga hatua katika uwezekano wa mauzo ya ndege 60 za kijeshi chapa Rafale, amesema kuwa ana imani mataifa ya Kiarabu ya eneo la ghuba pia yatasaidia kampeni inayofanyika nchini Mali.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema Ujerumani haitashiriki katika kupeleka jeshi nchini Mali lakini itasaidia katika masuala ya kimbinu.
"Inawezekana baadaye tukasaidia usafirishaji wa majeshi, na pia kutoa msaada wa kimbinu, kisiasa, kiutu ama dawa kwa majirani zetu Ufaransa na marafiki zetu".
Akijibu swali kutoka kwa waandishi habari katika ziara ya Umoja wa falme za Kiarabu, waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, ameongeza kuwa kuwapo majeshi ya Ufaransa katika nchi ambayo ni ya Kiislamu katika bara la Afrika hakutaongeza nguvu za kundi la al-Qaeda kupata wafuasi zaidi kutoka katika eneo hilo.
Wakati huo huo, wapiganaji wa kundi la Taliban nchini Afghanistan wameshutumu leo jeshi la Ufaransa kuingilia kati mzozo wa Mali, likionya kuwa hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya. Taliban imesema katika tovuti yake kuwa Ufaransa inapaswa kujifunza kutokana na kushindwa kwa vita nchini Afghanistan na Iraq.
Mataifa ya magharibi pamoja na mataifa jirani yana hofu kuwa wapiganaji wa Mali wataitumia ardhi ya nchi hiyo kama sehemu ya kufanyia mashambulizi yao dhidi ya mataifa ya kigeni.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri:Josephat Charo