1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yapitisha kodi dhidi ya makampuni ya kiteknolojia

11 Julai 2019

Baraza la Seneti la Ufaransa limeidhinisha kodi kwa kampuni za masuala ya kiteknolojia, hatua inayoelekea kuanzisha vita vya kibiashara kati ya Washington na Umoja wa Ulaya, huku Marekani ikianzisha uchunguzi.

Versailles Emmanuel Macron Rede
Picha: Reuters/C. Platiau

Siku ya Jumatano (Julai 10), Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru uchunguzi juu ya kodi hiyo, ambayo inaweza kuifanya Marekani nayo kuweka ongezeko la ushuru au vikwazo vyengine vya kibiashara.

"Kati ya washirika, tunapaswa na tunaweza kutatua mivutano yetu sio kwa vitisho, bali kwa njia nyengine," aliSema Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire, kabla ya kura hiyo kupigwa leo (Julai 11).

Asilimia tatu ya ushuru itatozwa kwa huduma za kidijitali kutoka kwenye makampuni yenye mapato ya zaidi ya euro milioni 25 ndani ya Ufaransa na euro milioni 750 kutoka kwengine duniani. Ushuru huo unatazamiwa kuanza kazi mara tu kalenda ya bajeti itakapoanza mwaka huu wa 2019. 

Ufaransa iliamua kuendelea na kodi hiyo baada ya mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kushindwa kukubaliana juu ya kiwango kinachofaa yakikabiliwa na upinzani mkali kutoka Ireland, Denmark, Sweden na Finland.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasema kodi hiyo ni kwa ajili ya haki za kijamii.Picha: Reuters/C. Platiau

"Ufaransa ni taifa huru, uamuzi wake juu ya masuala ya kodi ni huru na utaendelea kuwa huru," alisema Le Maire.

Mataifa zaidi yajipanga kutoza kodi

Mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya zikiwemo Austria, Uingereza, Uhispania na Italia nazo pia zimetangaza mipango ya kuanzisha kodi zao wenyewe za masuala ya kidijitali. 

Nchi hizo zinasema kodi hiyo inahitajika kwa kuwa makampuni ya mtandao wa intaneti ya kimataifa, kama vile Facebook na Amazon, zinaweza sasa uandikisha faida yake katika mataifa yenye kiwango cha chini cha kodi kama vile Ireland, bila kujali mapato hayo yametokea nchi gani.

Shinikizo la kisiasa kujibu hatua hiyo limekuwa likiongezeka huku watumiaji wa rejareja kwenye mitaa mikubwa na mitandaoni wakijikuta wanapoteza; Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa kuyatoza kodi makampuni makubwa ya teknolojia ni suala la haki za kijamii.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha wa Ireland Paschal Donohoe alisema mwezi Mei kwamba kodi zinazolenga zaidi makampuni ya kidijitali ya Marekani "zitachochea zaiid wasiwasi wa biashara duniani na kuathiri biashara na uwekezaji unaovuuka mipaka," na ingekuwa vigumu kufikia makubaliano juu ya mageuzi duniani.