Ufaransa yasema mazungumzo ndio njia ya ufumbuzi nchini Libya
11 Julai 2011►
Waziri wa ulinzi Gérard Longuet ameshurutisha kumalizika opereshini za kijeshi zinazoongozwa na jumuiya ya kujihami ya NATO na kuanzishwa mazungumzo kati ya wanaharakati wanaomuunga mkono Gaddafi na upande wa upinzani.
Waziri wa ulinzi wa Ufaransa amezungumzia juu ya "kuendelea kuwepo Muammar Gaddafi akiwa na cheo kingine" huku akikumbusha "kuna baadhi ya wananchi wake wanaotaka ang'atuke.
"Baada ya miezi minne ya hujuma za kijeshi nchini Libya,wakati umewadia wa kusaka ufumbuzi wa kisiasa" amesema waziri huyo wa ulinzi wa Ufaransa kupitia kituo cha televisheni cha nchi hiyo BFM-TV.
Waziri mwenzake wa mambo ya nchi za nje ,Alain Juppé akihojiwa na kituo cha televisheni cha France Info amesema kwa upande wake na hapa tunanukuu:" utaratibu unabidi uanze kwa kuwekwa chini silaha,chini ya usimamizi wa Umoja wa mataifa.
Na yeye pia amezungumzia juu ya kuanzishwa mazungumzo kati ya baraza la mpito na wale aliowaita "viongozi wa Libya na hasa wale wa Tripoli waliotambua enzi za Gaddafi zimekwisha.
Kwa maoni ya mwanadiplomasia mkuu wa Ufaransa kishindo kilichopo kwasasa ni namna ya kumtenganisha Gaddafi na madaraka yote ya kisiasa na kijeshi.
Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani haijakawia kujibu msimamo huo mpya wa Ufaransa.Katika taarifa yake,wizara hiyo ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema "ni jukumu la walibya wenyewe kuamua kipindi cha mpito kiwe cha aina gani."Imesisitiza hata hivyo msimamo wake dhidi ya kuendelea kuwepo madarakani Gaddafi.
Katika mahojiano pamoja na gazeti la Algeria Al Akhbar,toleo la leo,mtoto wa kiume wa Muammar Gaddafi,Seif Al Islam amezungumzia mazungumzo yanayoendelea kati ya maafisa wa serikali ya Libya na serikali ya Ufaransa."Mjumbe tuliemtuma kwa Sarkozy amesema rais wa Ufaransa ,amemwambia wazi kabisa "wao ndio waliounda baraza la waasi,na bila ya msaada wao,fedha zao na silaha zao baraza hilo lisingekuwepo"amesema Seif al Islam . na kuongeza Ufaransa imesema "wakifikia makubaliano pamoja na Tripoli,basi watalilazimisha baraza la mpito liweke chini silaha."Mwisho wa kumnukuu Seif al Islam.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters
Mhariri Yusuf Saumu
◄