1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yatinga fainali baada ya kuibwaga Moroko 2-0

15 Desemba 2022

Mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa, wameihitimisha hadithi ya matumaini ya Afrika kuingia kwenye fainali baada ya kuibwaga Moroko 2-0 kwenye nusu fainali ikisalia hatua moja tu kutwaa kombe hilo tena.

WM Katar 2022 | Halbfinale | Frankreich vs Marokko
Picha: Peter Cziborra/REUTERS

Kama ilivyokuwa kwenye robo fainali na England, ndivyo ilivyokuwa kwenye nusu fainali hii na Moroko, na sasa kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, na wachezaji wake, wanajuwa kinachopaswa kufanywa wakati wakikutana na Argentina siku ya Jumapili (Disemba 18) kwenye fainali yao ya tatu. 

Akizungumza na kituo cha TF1 baada ya mchezo, Deschamps alisema kwamba hisia ni za juu sana, kama ilivyo fakhari ya ushindi wenyewe.

"Hii ilikuwa hatua nyengine muhimu lakini bado kuna moja iliyobakia. Tumekuwa pamoja kwa mwezi  mzima sasa, haikuwa rahisi, lakini hadi sasa mambo ni mazuri na wachezaji wangu wamezawadiwa." Aliongeza kocha huyo.

Hata hivyo, wachambuzi wa soka wanasema ni Morokondiyo iliyobeba hadithi nzima ya Kombe la mwaka huu.

Licha ya kukutwa na mshangao wa bao la kwanza katika dakika ya tano tu ya mchezo, kamwe haikuonekana kulemewa na muda wote wachezaji walisalia na nishati na hamasa ile ile ya kutaka kuiinuwa bendera ya Afrika kwenye Kombe la Dunia. 

Kylian Mbappe wa Ufaransa akimfariji rafiki yake, Achraf Hakimi, wa Moroko baada ya Ufaransa kushinda 2-0 na kuingia fainali.Picha: Manu Fernandez/AP Photo/picture alliance

Wakisaidiwa na maelfu ya mashabiki waliojazana uwanjani, Simba hao wa Atlas walifanya kila wawezalo kurejesha na kushinda, hadi dakika ya 79 pale Randal Kolo Muani alipopachika bao la pili na la mwisho kwa Ufaransa.

Tunakwenda kujinowa upya - Regragui

Kocha wa Moroko, Walid Regragui, alisema baada ya mchezo kwamba wachezaji wake walijitolea kadiri ya uwezo wao.

"Wamekwenda umbali walioweza kufika. Sasa ni ngumu kusonga mbele zaidi hapa kwao. Walitaka kuandika historia, lakini huwezi kushinda Kombe la Dunia kwa miujiza. Unashinda kwa kufanya kazi kubwa na hicho ndicho tunachokwenda kukifanya sasa, kuendelea kufanya kazi kubwa." Aliongeza kocha huyo wa Moroko.

Walid Regragui, kocha wa Morocco.Picha: NurPhoto/IMAGO

Hata baada ya mchezo kumalizika kwa kubwaga 2-0, mashabiki wa Moroko ndani na nje ya uwanja walisema wazi kwamba wao ndio washindi wa michezo ya mwaka huu hata kama sio watakaobeba kombe.

"Ni Moroko iliyoonesha maajabu kufika ilipofika na sio Ufaransa, ambayo ni mabingwa watetezi." Walisema.

Moroko imeandika historia

Tayari Moroko ilishaandika historia kwa kuungana na Marekani na Korea Kusini kuwa timu pekee nje ya mabara mawili yanayotawala soka la dunia, Ulaya na Amerika ya Kusini, kufika umbali huu.

Ilifanikiwa kuibana Croatia iliyowahi kufika fainali mwaka 2018, ikaibwaga Ubelgiji na kisha kuzitowa Uhispaniana Ureno. 

Wachezaji wa Moroko wakijifuta machozi baada ya kupoteza 0-2 kwa Ufaransa kuingia fainali ya Kombe la Dunia.Picha: Natacha Pisarenko/AP Photo/picture alliance

Chini ya Regragui, ambaye aliichukuwa timu hiyo miezi michache kabla ya michuano hii, Moroko inaondoka nchini Qatar ikiwa imejijengea heshima kutokana na kikosi chake. 

"Kwa miaka 20 sasa, unaweza kusema Ufaransa imekuwa kwenye kiwango cha juu cha soka duniani. Naona fahari kwa kuwa mwenyewe nikulia Ufaransa na nilijifunza mpira huko. Unaweza kuwakosoa makocha ama mpira wa Ufaransa, lakini wana wachezaji na makocha bora kabisa na timu bora kabisa duniani. Ikiwa Ufaransa itashinda kwenye fainali, litakuwa jamboo zuri maana kwetu tutasema tulishindwa na mabingwa." Alisema kocha huyo aliyekulia nchini Ufaransa.