1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yatinga nusu fainali mashindano ya EURO 2022

Josephat Charo
24 Julai 2022

Kocha wa Ufaransa Corinne Diace amesema timu yake inashiriki mashindano ya EURO kujenga historia yao baada ya kufuzu kwa nusu fainali kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Uholanzi Jumamosi (23.07.2022)

UEFA I Women 2022 I Niederlande v Frankreich
Picha: Eibner/Memmler/IMAGO

Kocha Corinne Diarce amesema Les Bleues hawajatosheka kwa kupiga hatua mpya na kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza katika mashindano ya EURO ya wanawake kwa kuwapiku mabingwa watetezi Uholanzi 1-0 katika muda wa ziada.

Eve Perisset alifunga kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 102 katika muda wa ziada na kuiwezesha Ufaransa kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza kufikia hatua hiyo katika mashindano ya kombe la EURO kwa wanawake. Ufaransa itakwaana na Ujerumani katika kipute cha nusu fainali Jumatano Julai 27. Ufaransa hawajawahi kuingia fainali ya mashindano makubwa.

"Hiyo si historia yetu, tuko hapa kutengeneza historia yetu," alisema Diarce. "Wachezaji hapa pamoja na wasimamizi wa timu, sote tunataka kuandika historia yetu wenyewe. Bado kuna safari ndefu kidogo. Tumefikia kiwango kipya usiku wa leo lakini si mwisho," aliongeza kusema Diarce ambaye alikosolewa vikali kwa kuchangia Ufaransa kufungishwa virago katika hatua ya robo fainali nyumbani katika michuano ya kombe la dunia la kandanda miaka mitatu iliyopita. "Tunataka kufika fainali." Alisema Diarce.

Ufaransa ilitawala sehemu kubwa ya mchezo ikipiga mikwaju 33 iliyolenga lango ikilinganishwa na mikwaju tisa ya wapinzani wao, lakini kipa wa Uholanzi Daphne van Demselaar aliwanyima fursa ya kutetemesha kamba. Matokeo ya mechi hayakukitendea haki kiwango cha mchezo kilichooneshwa na timu zote mbili huku Ufaransa ikitolewa kijasho na kukatishwa tamaa kwa dakika 90 na umahiri wa kipa Daphne.

Kipa wa Uholanzi, Daphne van Domselaar, aliokoa mabao ambayo yangetiwa kimyani na WafaransaPicha: Tim Goode/IMAGO

"Ulikuwa mchezo mrefu jioni hii," alisema kocha wa Ufaransa Diarce. "Tulitamani tuwe tumefunga mapema lakini tulikabiliana na mlindalango mahiri wa Uholanzi."

"Kuhusu uwezo wetu wachezaji wametoa majibu mengi sana jioni ya leo na katika safu ya ulinzi pia tumetoa majibu mengi. Hatukutoa majibu katika safu ya ushambuliaji katika kutumia mbinu lakini tumetengeneza fursa kadhaa na kukaribia kufunga."

Mshambuliaji Selma Bacha, mchezaji bora wa mechi wa EUFA, amesema, "Kama wachezaji uwanjani hatukuwa na shaka. Nadhani timu ilikuwa sawa, imekamilika jioni hii hakuna cha kuongezea."

"Kulikuwa na sherehe katika chumba cha kubadilishia nguo baada ya mechi, tutafurahia muda huu wa ushindi na kesho tutakuwa katika hali ya mapumziko na kupona."

Uholanzi walijikakamua hadi dakika ya mwisho

Uholanzi imekabiliwa na majeruhi huku mlindalango nambari moja Sari Van Veenendaal akishindwa kucheza katika mashindano ya mwaka huu huku maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 yakimkumba Vivianne Miedema na Jackie Groenen. Sari aliumia bega katika mechi ya ufunguzi na Sweden.

Miedema alikuwa fit kurejea uwanjani baada ya kukosa mechi za makundi walizoshinda dhidi ya Ureno na Uswisi kutokana na ugonjwa wa Covid. Hata hivyo mshambuliaji huyo wa klabu ya Arsenal alionekana na mapungufu katika uwezo wake huku mchezaji huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji bora kabisa wa kandanda duniani akipambana kutoa mchango wa kuonekana katika mechi hiyo.

Kocha mkuu wa Uholanzi Mark Parson ana fahari kwa jinsi timu yake ilivyocheza katika kukabiliana na upinzani mkali. "Tumekuwa na changamoto nyingi, matatizo mengi, upinzani mkali lakini sikuhisi sababu za kujitetea zikitolewa kutoka kwa wachezaji," alisema.

"Mwishowe, tulikuwa tunalazimika kubadilisha timu kila mechi kwa sababu ya matatizo na ungeweza kuona mawasiliano ya kiwango cha kandanda letu hayakuwa juu kama tulivyotaka yawe katika pambano la robo fainali."

"Kwa sababu ya nguvu na mapambano na moyo wa wachezaji hawa tumeufanya mchezo kuwa mgumu sana."

(reuters, afp)