1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufichuaji mkubwa akaunti za siri za matajiri

Admin.WagnerD4 Aprili 2016

Viongozi wa dunia, nyota wa michezo na filamu ni miongoni mwa matajiri kadhaa waliotajwa katika kile kinachoweza kuwa ufichuaji mkubwa zaidi wa taarifa za ndani katika historia.

Panama Papers
Picha: picture alliance/maxppp

Ufichuaji huo mkubwa unaohusisha nyaraka milioni 11.5, na kupewa jina la "Panama Leaks" umeonyesha namna matajiri wanavyotumia maeneo salama ya kodi kuficha utajiri wao na kukwepa kodi.

Uchunguzi uliyofanywa na zaidi ya makampuni 100 ya habari umefichua mali zilizofichwa nje za watu mashuhuri duniani, wakiwemo wanasiasa karibu 140.

Nyaraka hizo zilipatikana na gazeti la kila siku la nchini Ujerumani - Süddeutsche Zeitung na kusambazwa kwa makampuni mengine ya habari ulimwenguni na jukwa la kimataifa la waandishi wa habari za uchunguzi ICIJ.

Nyaraka hizo zinazoyahusu mashirika karibu 214. 000 ya nchi za kigeni kwa muda wa karibu miaka 40, zilitoka kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca, yenye makao yake nchini Panama - na ikiwa na ofisi katika mataifa zaidi ya 35.

Jengo la kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca katika mji mkuu wa Panama - Panama City.Picha: picture alliance/AP Photo/A. Franco

Putin, Xi Jinping, Jackie Chan watajwa

Uchunguzi huo unadai kuwa washirika wa karibu wa rais wa Urusi Vladmir Putin, ambaye binafsi hajatajwa katika nyaraka hizo za siri, walihamisha kwa siri kiasi cha dola bilioni mbili kupitia mabenki na makampuni hewa.

Viongozi 12 walioko madarakani na wa zamani pia wametajwa katika uchunguzi huo, wakiwemo waziri mkuu wa Pakistan, rais wa Ukraine na Mfalme wa Saudi Arabia, na vile vile nyota wa filamu akiwemo Jackie Chan.

Wachunguzi wamedai pia kuwa familia ya rais wa China Xi Jinping ina mahusiano na akaunti za nje, kama alivyokuwa marehemu baba wa waziri mkuu wa sasa wa Uingereza David Cameron, na wanadai pia kuwa waziri mkuu wa sasa wa Iceland aliwekeza kwa siri, mamilioni ya pesa kwenye benki za nchi hiyo wakati wa mgogoro wa kifedha.

Mkurugenzi wa jukwaa la kimataifa la waandishi wa habari za uchunguzi Gerard Ryle amesema kinachoshtua zaidi ni namna ulimwengu wa nje unavyotumiwa na viongozi walioko madarakani, ambao baadhi yao wamekuwa wakijitanabisha kuwa wapinzani wakubwa wa usiri.

"Tunachopaswa kufanya hapa kama waandishi habari ni kuvunja usiri kwa sababu bodhaa pekee inayotolewa na ulimwengu wa nje ni usiri, na bila hivyo basi hakutakuwa tena na bidhaa hivyo kadiri tunavyoendelea kuwafedhehesha watu, nadhani tutaona mageuzi ya kweli," alisema Ryle katika mahojiano na DW.

Wateja wa Mossack Fonseca

Kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca ilifanya kazi na watu wasiopungua 33 na makampuni yliyoorodheshwa na Marekani kwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na magenge ya wauza madawa ya kulevya nchini Mexico, makundi ya kigaidi na mataifa sugu, ikiwemo Korea Kaskazini. Moja ya makampuni hayo lilitoa mafuta kwa ajili ya ndege za utawala wa Syria zilizotumiwa kuwashambulia wake.

Ufichuzi wa Panama unatajwa kuwa mkubwa zaidi katika historia.

Wateja wa kampuni hiyo wanahusisha wawekezaji wa uongo, magwiji wa madawa, wakwepaji kodi, na mfanyabiashara wa Marekani alitiwa hatiani kwa kwenda nchini Urusi kufanya ngono na watoto yatima walio chini ya umri, ambaye alisaini nyaraka za za kampuni ya nje akiwa gerezani.

Lionnel Messi, Sepp Blatter nao wamo

Nyaraka hizo pia zinahusisha matajiri 29 walioko katika orodha ya matajiri ya jarida la Forbs, na nyota wa filamu za mapigano Jackie Chan. Yumo pia mjumbe w akamati ya Maadili ya FIFA Juan Pedro Damian, mchezaji soka nambari moja duniani Lionnel Messi na rais wa zamani wa FIFA Sepp Blatter.

Zaidi ya benki 500 na benki zake tanzu na matawi pia zimefanya kazi na kampuni ya Mossack Fonseca tangu miaka ya 1970 kuwasaidia wateja wao kusimamia makampuni ya nje.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri. Saumu Yusuf

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi