Ufichuzi kuhusu Pagasus na kashfa kubwa ya udukuzi
23 Julai 2021Kupitia programu hiyo ya Udukuzi namba zaidi ya 50,000 za simu zimebainika kuwa kwenye orodha ya udukuzi unaofanywa na kampuni ya Israel ya teknolojia ya ujasusi NSO ambayo ndiyo iliyotengeneza programu ya udukuzi ya Pegasus.
Timu ya mtandao wa habari za uchunguzi ilifanikiwa kugundua kwamba miongoni mwa waliolengwa katika udukuzi wa NSO ni pamoja na waandishi habari,wanaharakati wa haki za binadamu,mameneja wa makampuni na wanasiasa kiasi 600 na maafisa wa serikali kutoka nchi zaidi ya 50.
Programu hiyo ya udukuzi inauwezo wa kuwasha kamera au sauti na kurekodi mawasiliano yote ikiwemo kusoma kila ujumbe wa simu na kila kitu kinachofanyika kwenye simu yako ya mkononi.
Kisichofahamika wazi bado ni ikiwa watu ambao data zao simu zilikuwa kwenye orodha ya NSO wamedukuliwa au la.
Miongoni wa watu ambao wamelengwa katika kadhia hii ya udukuzi ni wanasiasa wa ngazi za juu katika Umoja wa Ulaya kama vile waziri mkuu wa zamani wa Ubelgiji na rais wa sasa wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel. Na hata nambari ya simu ya baba yake Louis Michel iko kwenye orodha ya NSO.
Hata rais wa Ufaransa naye yumo kwenye orodha
Kiongozi mwingine maarufu aliyetajwa katika orodha hiyo ni rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,nambari yake ya simu iliyoorodheshwa amekuwa akiitumia tangu mwaka 2017 na ambayo bado alikuwa anapatikana kwa nambari hiyo hadi siku chache zilizopita,kwa mujibu wa gazeti maarufu la Ufaransa, Le Monde.
Kadhalika nambari ya mmoja wa walinzi wake wa zamani sambamba na waziri mkuu wa zamani Phillipe,waziri wa mambo ya nje Jean Vye Le Drian na waziri wa uchumi Le Maire.
Serikali ya Ufaransa kwahivyo imekasirishwa sana na kadhia hii. Msemaji wa serikali iyo Gabriel Attal amesema wameshtushwa sana na ripoti hii ya ufichuzi iliyochapishwa na waandishi habari na ikiwa yaliyochapishwa yatabainika kuwa ya kweli basi hatua kali zitachukuliwa.
Morroco ndiyo inayotajwa kuhusika kuwadukua wanasiasa wa Ufaransa na rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel.
Ubalozi wa Morrocco mjini Paris lakini umekanusha tuhuma zinazotolewa dhidi ya nchi yake.
Aidha inaelezwa kwamba kiasi nambari za simu 15,000 kwenye orodha ya NSO ni za Wamexico ikiwemo ya rais wa nchi hiyo Andres Manuel Lopez Obrador pamoja na baadhi ya nambari za wanafamilia yake na watu wanaomzunguuka.
Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani ameibebesha lawama serikali iliyopita kuhusu kadhia hii.
Udukuzi kutoka kila pembe ya ulimwengu
Lopez Obrador aliingia madarakani mwaka 2018 na Mexico ni nchi ya kwanza kununua programmu ya ujasusi ya Pegasus mnamo mwaka 2011.Kwa maneno mengine kuuwawa kwa mwandishi habari wa kimexico Cecilio Pineda Birto aliyepigwa risasi mwaka 2017 inawezekana kukahusishwa na kadhia ya Pegasus.
Birto kwa kipindi kirefu alijihusisha kuripoti juu ya ufisadi na mtandao wa mafia wa biashara ya mihadarati. Nambari yake pia imekutwa kwenye orodha ya udukuzi. pamoja na nambari jumla ya 26 za waandishi habari wa Mexico.
Nambari za waandishi habari jumla 180 duniani zimo kwenye orodha hiyo ikiwemo ya aliyekuwa mwandishi habari wa Kisaudi Jamal Khashoggi aliyeuliwa katika ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul Uturuki.
Israel imesema inaunda jopo kazi litakalofanya uchunguzi wa kadhia hii inayohusu kampuni yake ya teknolojia ya ujasusi NSO na jopo hilo litaongozwa na baraza la kitaifa la usalama ambalo linaripoti moja kwa moja kwa waziri mkuu Natfali Bennett.