1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufilipino, taifa la majanga ya asili

11 Novemba 2013

Kimbunga Haiyan ni mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya asili kuwahi kuikumba Ufilipino, lakini siyo janga pekee, nchi hiyo ya Kusini mwa Asia iko katika eneo linalokabiliwa na kitisho kikubwa cha vimbunga.

Picha: Reuters

Ufilipino imeathirika kutokana idadi kubwa ya vimbunga, matetemeko ya ardhi, milipuko ya volcano na majanga mengine ya asili. Hii ni kwa sababu iko katika ukanda wenye hatari ya kutokea vimbunga, au Ring of Fire katika Kiingereza, ambalo ni eneo kubwa la Bahari ya Pasifik ambako hutokea milipuko mingi ya volcano pamoja na matetemeko ya ardhi. Kila mwaka, karibu vimbunga 80 hutokea katika maziwa ya Kitropiki, ambapo 19 kati ya vimbunga hivyo huingia katika eneo la Ufilipino na sita hadi tisa hupiga katika nchi kavu, kwa mujibu wa Kituo cha Pamoja cha Tahadhari za Vimbunga.

Ufilipino ndio nchi inayokabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na vimbunga vya Kitropiki kote ulimwenguni. Na vimbunga vikubwa kama hiki cha hivi karibuni cha Haiyan, vinaweza kutengeneza nishati mara kumi zaidi ya bomu la atomiki la Hiroshima. Hii hapa orodha ya matetemeko ya ardhi, milipuko ya volcano, vimbunga na majanga mengine ya asili ambayo Ufilipino imekumbana nayo katika mwongo mmoja uliopita, na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na kuharibu kabisa miundo mbinu na uchumi wa nchi hiyo.

Wakaazi wakirusha vifaa kutoka duka moja, katika mji wa Guiuan, wa mkoa wa mashariki wa SamarPicha: Reuters/Ted Aljibe

Tetemeko la ardhi Bohol Oktoba 2013

Mnamo Oktoba 15, 2013 mkoa wa kisiwa cha Bohol, katikati ya eneo la Visayas nchini Ufilipino, ulikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi kuwahi kutoka Ufilipino katika miaka 23. Tetemeko hilo lilidumu sekunde 34 na likawa na ukubwa wa 7.2 kwenye vipimo vya Richter. Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga, watu 222 waliaga dunia, 976 wakajeruhiwa na zaidi ya nyumba 73,000 zikaharibiwa au kuteketezwa. Inakadiriwa kuwa kiwango cha nishati ambayo tetemeko hilo lilitengeneza, ni sawa na mabomu 32 ya Hiroshima.

Kimbunga Bopha, Novemba – Desemba 2012'

Kimbunga kikali cha Bopha kilitokea Desemba 3, 2012, katika kisiwa cha Kusini mwa Ufilipino cha Mindanao, ambacho kilikuwa kimeharibiwa na dhoruba ya Washi mwaka mmoja uliotangulia. Kimbunga Bopha kilisababisha uharibifu mkubwa na kuwauwa watu 600. kiwango cha uharibifu kilikadiriwa kufikia euro milioni 749.

Mkaazi akiwa amebeba bendera ya taifa iliyoraruka, akiwa kwenye vifusi vya mji wa HernaniPicha: Reuters/Afp/Ted Aljibe

Maporomoko ya ardhi ya Pantukan, Januari 2012

Jamii ya wachimba migodi ya mji wa Pantukan katika kisiwa cha kusini mwa Ufilipino cha Mindanao ilikabiliwa na kitisho kikubwa cha kutokea maporomoko ya ardhi. Kwa ajili ya milima na mabonde, na isiyo na miti ya kutosha, kabla ya kukumbwa na mkasa huo mnamo Januari 5, 2012. Watu 25 waliuawa wakati maporomoko ya ardhi yalipotokea katika mgodi wa dhahabu karibu na mji huo.

Kimbunga cha Kitropiki Washi, Desemba 2011

Kimbunga cha Kitropiki Washi kilisababisha mafuriko ya ghafla ambayo yalielekea maeneo ya chini ya milima, na kung'oa miti, mito kufurika, yote hayo yakifanyika wakati wakaazi wakiwa usingizini. Kilisababisha vifo vya watu 1,080 na kuharibu miji ya pwani ya Cagayande Oro na Iligan, na kuigeuza kuwa vifusi vya magari yaliyobondeka, ma mizoga ya wanyama. Nyumba walizokuwa wamelala watu zilisombwa na maji hadi baharini katika eneo hilo la Ufilipino ambalo halina uwezo wa kupambana na vimbunga. Ilichukua miezi kadhaa ili kurudisha umeme na maji katika eneo hilo.

Kimbunga Fengshen, Juni 2008

Kimbunga Fengshen, kilichofahamika pia kama kimbunga “Frank”, kilisababisha uharibifu mkubwa Ufilipino, kuanzia Juni 20 hadi Juni 23, 2008, na kuwauwa watu 557. kiliziathiri karibu familia 99,600 kote Ufilipino, na kuharibu zaidi ya nyumba 155,000 katika maeneo 10. Baraza la Ufilipino la Kupamba na Mikasa lilikadiria kuwa uharibifu wa kilimo na uvuvi ulifikia hasara ya euro milioni 57.2, miundo mbinu euro milioni 3.7 na boti za uvuvi euro milioni 1.9.

Meli hii ya mizigo ilisombwa na maji na kuwekwa kutupwa ufukweniPicha: Reuters/Romeo Ranoco

Kimbunga Durian, Novemba 2006

Mnamo Novemba 25, 2006, kimbunga “Durian” kiliipiga Ufilipino, na kuharibu nyumba, kung'oa miti na kuwaua watu 720. kutokana na mvua kubwa, mjji wa Legazpi ulilazimika kukabiliana na mafuriko makubwa wakati maporomoko ya udongo kutoka mlima wa Volkano wa Mayon yakivifunika vijiji vingi, na kusababisha vifo vya watu wengine 800 hadi 1,000. Baada ya kuipiga Ufilipino, kimbunga Durian kilielekea katika bahari ya Kusini ya China na kuipiga Vietnam muda mfupi baadaye.kimbunga hicho kilisababisha vifo vya karibu watu 2,000 na mamia ya wengine hawakujulikana waliko. Uharibifu nchini humo ulikadiriwa kuwa euro milioni 97.

Maporomoko ya ardhi ya Guinsaugon, Februari 2006

Kijiji cha Guinsaugon, sehemu ya kusini mwa kisiwa cha Leyte, kilifunikwa wakati upande mzima wa mlima ulipoporomoka mnamo Februari 17,2006, na kuwaua watu 1,126.

Wakaazi wakiokota baadhi ya vitu vilivyobaki kwenye vifusi vya nyumba zilizoporomokaPicha: Reuters

Shule moja pamoja na makaazi 500 yalifunikwa wakati udongo ulipoporomoka kutoka juu mlimani. Mkasa huo ulitokea baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo kwa siku kumi mfululizo. Wenyeji wanalaumu uharibifu wa misitu, unaosababishwa na ukataji miti kinyume cha sheria, kuwa sababu iliyochangia katika janga hilo.

Kimbunga Winnie, Novemba 2004

Ijapokuwa Winnie kilizingatiwa tu kuwa kimbunga cha Kitropiki, kilisababisha vifo vya watu 842 nchini Ufilipino, wakati wengine 751 wakakosa kujulikana waliko. Uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho ambacho kiliipiga Ufilipino mwishoni mwa Novemba 2004, ulikadiriwa kuwa euro milioni 11.8. muda mfupi baada ya Winnie kusababisha uharibifu mkubwa, Ufilipino ilipigwa na kimbunga kingine kikali zaidi kwa jina “Nanmadol” ambacho kiliwaua watu 70.

Mwandishi: Bruce Amani/Jessie Wingard, Anne-Sophie Brändlin

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW