1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroChina

Ufilipino yaishutumu China kutaka kupoka eneo la bahari

11 Mei 2024

Ufilipino imesema leo kuwa imepeleka meli zake katika eneo linalozozaniwa la Bahari ya China Kusini ambapo imeishutumu China kwa kujenga "kisiwa bandia" katika mzozo wa bahari unaozidi kutanuka.

Meli ya China ikijaribu kuizuia meli ya ufilipino
Eneo la bahari la kusini mwa China limekuwa chanzo cha mzozo na makabiliano kati ya meli za China na Ufilipino.Picha: Adrian Portugal/REUTERS

Katika taarifa, ofisi ya Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr, imesema kuwa walinzi wa Pwani wametuma meli kufuatilia kile kinachodaiwa kuwa shughuli haramu za China, za kuunda "kisiwa bandia", na kuongeza kuwa meli nyingine mbili hupelekwa kwa zamu katika eneo hilo.

Msemaji wa walinzi wa Pwani ya Ufilipino Commodore Jay Tarriela, ameliambia kongamano moja kuwa kumekuwa na uboreshaji wa kiwango kidogo wa eneo la bahari la Sabina Shoal,  na kwamba huenda China ndio iliyohusika katika uboreshaji huo .

Ubalozi wa China mjini Manila haukujibu mara moja ombi la tamko kuhusu madai hayo ya Ufilipino, ambayo huenda yakaongeza tofauti zilizoko baina ya nchi hizo mbili.