Ufilipino yapandisha umri wa ridhaa ya ngono kuwa miaka 16
7 Machi 2022Taifa hilo lenye Wakatoliki wengi lilikuwa na umri wa chini kabisa wa ridhaa ya kujamiiana duniani, likiwaruhusu watu wazima kufanya mapenzi na watoto wenye umri wa miaka 12 iwapo wangekubali.
Chini ya sheria iliyorekebishwa na iliyotiwa saini na Rais Rodrigo Duterte siku ya Ijumaa na kuwekwa hadharani Jumatatu, kufanya mapenzi na mtu aliye chini ya miaka 16 itakuwa kinyume cha sheria na adhabu yake itakuwa kifungo cha miaka 40 jela. Sheria hiyo haitowahusu wapenzi ambao wote ni vijana ili mradi tofauti yao ya umri isizidi miaka mitatu na kuwepo makubaliano kuhusu kitendo cha ngono.
Soma pia: Watu waliokufa kutokana na kimbunga Ufilipino yafikia 388
Margarita Ardivilla, mtaalamu wa ulinzi wa watoto katika shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF nchini Ufilipino amesema kuwa sheria hii ni chombo kizuri sana cha ulinzi kwa watoto dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, iwe unaanzia mtandaoni au kukutana ana kwa ana. Ameendelea kuwa, ni muhimu sana kuwa na umri uliyo wazi wa kuamua ubakaji kisheria na kwamba sheria ya chini ya miaka 12 ya mwaka 1930 haikuwa halali.
Wanaharakati wa haki za watoto wamekuwa wakishinikiza kwa miongo kadhaa kuongeza umri wa ridhaa ya ngono, lakini kanuni za kijamii zilizokita mizizi katika nchi hiyo yenye udini ambapo utoaji wa mimba na talaka ni kinyume cha sheria zimekuwa zikikatisha juhudi zao.Bunge liliidhinisha mswada huo mwezi Desemba.
Ufilipino inayokumbwa na umaskini imekuwa sehemu kuu duniani ya vitendo vya unyanyasaji wa watoto kingono mtandaoni na data rasmi inaonyesha kuwa takriban wasichana 500 wenye umri kati ya miaka 10-19 hujifungua kila siku.
Soma pia: Jumuiya ya ASEAN yaadhimisha miaka 30 ya uhusiano wake
Ubakaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia pia umekithiri
Utafiti wa UNICEF ulioungwa mkono na serikali na kufanyika nchini kote mwaka 2015, ulionyesha kuwa mtoto mmoja kati ya watano wenye umri wa miaka 13-17 alifanyiwa ukatili wa kijinsia, na mmoja kati ya 25 alibakwa utotoni.
Rowena Legaspi, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Haki za Kisheria na Maendeleo ya Watoto anasema sheria hii inatoa ujumbe mzito sana kwamba ubakaji wa watoto ni uhalifu wa kutisha na lazima uadhibiwe ipasavyo.
Sheria hiyo inatoa ulinzi sawa kwa wavulana na wasichana, na imeitaka idara ya elimu kujumuisha masomo yanayoendana na umri kuhusu haki za watoto katika mtaala wa shule za msingi. Hata hivyo, wanaharakati walionya kuwa sheria hiyo itafanya kazi ya kuwaadhibu wakosaji au kuwazuia wanaotaka kufanya vitendo vya unyanyasaji ikiwa itatekelezwa ipasavyo.
Junice Melgar, mkurugenzi wa Kituo cha Afya ya Wanawakecha Likhaan anasema ameipokea vyema hatua hiyo lakini ana wasiwasi kama kutakuwepo utekelezaji.
Soma pia: Waandishi habari kutoka Ufilipino, Urusi washinda tuzo ya amani ya Nobel
Mwaka jana, Rais Duterte alitangaza kuwa, kuzuia mimba za utotoni kuwa ni kipaumbele cha taifa, akitaja ongezeko la hatari ya matatizo ya kiafya kwa mabinti wanaopata ujauzito na watoto wao pamoja pia na ukosefu wa mapato.
Mwezi Januari, Duterte alitia saini mswada wa sheria wa kupiga marufuku ndoa za utotoni katika nchi ambayo msichana mmoja kati ya sita huingia kwenye ndoa kabla ya umri wa miaka 18. Mswada mwengine tofauti ambao unalenga unyanyasaji wa kingono mtandaoni na unyanyasaji wa watoto bado unajadiliwa bungeni.
Chanzo: AFPE