Ufisadi - Tembo chumbani
6 Agosti 2013Ulaji rushwa ni jambo la kawaida miongoni mwa nchi nyingi za Kiafrika - walimu wanapokea rushwa ili kufanya udanganyifu katika matokeo ya mitihani; huku nao wanasiasa wakifadhli kampeni zao kwa njia za ufisadi. Kwa upande mwengine, jeshi la polisi hufumbia macho uvunjwaji wa sheria za barabarani baada ya kupewa ‘kitu kidogo’. Wengi wanaamini kuwa rushwa ndio njia pekee ya mkato ya kujikwamua unapokumbwa na matatizo au kufanikisha jambo unalopania kulifanya. Lakini mwishowe, ulaji rushwa au malipo yasiyofungamana na sheria, huwa na athari kubwa kwa jamii na uchumi wa taifa lolote lile.
Dhamira ya Alfayo Odhiambo ni kuishi maisha ya uaminifu. Lakini bila ya yeye kufahamu, anajikuta kuwa ni sehemu ya kashfa ya nishati inayowahusisha wafanyabiashara wakubwa na wanasiasa wa ngazi ya juu. Alfayo hataki familia yake ihusishwe au jina lake lichafuliwe na sakata hili, na ndipo hapo anatafuta njia ya kujitoa na kujisafisha. Mkewe, Jennifer, ambaye ni mwalimu, pia anakabiliwa na hali hiyo hiyo shuleni kwake. Ulaji rushwa umekita mizizi shuleni humo. Lakini je, ataweza kuwa jasiri kupinga vishawishi hivi au ataangukia mtego wa rushwa?
Sasa tegemeo la familia ya Odhiambo ni rafiki yao Jeffrey, na shirika lake jipya la “Komesha Ufisadi Sasa”. Jeffrey hachelei kuchukua hatua kupambana na uovu huu, lakini je ataweza kustahimili joto la kisiasa baada ya kupuliza kipenga dhidi ya ufisadi?
Mchezo huu wa Noa Bongo Jenga Maisha yako kuhusu ufisadi kwa jina la “Tembo Chumbani” wenye sehemu kumi, unatufunza kwamba ingawa ni hatari kwa wanaopuliza kipenga dhidi ya ufisadi, bado inawezekana. Wasikilizaji pia wanajifunza kuwa ulaji rushwa una athari kubwa. Pia wanajifunza jinsi wanavyoweza kutimiza malengo yao bila ya kuchafua hadhi yao.
Noa Bongo Jenga maisha yako ni vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika idhaa sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.