1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufunguzi wa kivuko cha Rafah ni matumaini kwa Wapalestina

2 Februari 2026

Mkuu wa kamati ya wataalamu iliyoundwa kushughulikia uongozi katika Ukanda wa Gaza Ali Shaath amesema hatua ya Israel kufungua kivuko maalum cha Rafah ni ishara ya matumaini kwa wapalestina wanaoishi huko.

Misri Rafah 2026 | Kivuko cha Rafah kimefunguliwa tena baada ya kufungwa kwa mwaka mmoja
Kivuko cha Rafah kinachounganisha Misri na Ukanda wa Gaza upande wa Kusini Picha: Ahmed Sayed/Anadolu/picture alliance

Katika taarifa yake, Shaath amesema hatua hiyo ni mwanzo wa mchakato mrefu wa kuunganisha tena sehemu hiyo iliyofungwa takriban mwaka mmoja uliopita.

Kivuko hicho muhimu kinachopakana na Misri kusini mwa Ukanda Gaza kimefunguliwa leo huku Israel ikisema ni watu wachache tu wapatao 50 kila siku watakaoruhusiwa kukitumia.

Imeongeza kuwa wapalestina 42,000 pekee waliokimbia Gaza wakati wa vita ndio wataruhusiwa kurejea huko kupitia kivuko hicho.

Lakini kwa mujibu wa wizara ya afya kwenye Ukanda huo, kiasi cha wagonjwa 20,000 wanangojea kuingia Misri kwa matibabu, huku 440 kati yao wakiwa na hali mbaya kabisa. Wagonjwa 4,000 wa saratani na watoto 4,500 wamo pia kwenye orodha ya dharura.

Hata hivyo wapalestina wanatumai operesheni kupitia kivuka hicho itaendeshwa salama na kuridhia watu wengi zaidi kupita.

Kufunguliwa kwa kivuko hicho ni sehemu ya kile kiitwacho "mpango wa amani wa Rais Trump kwa Gaza".

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW