1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Ufyatuaji risasi kwa aliyekuwa mkuu wa ujasusi Sudan Kusini

22 Novemba 2024

Milio ya risasi ilirindima nyumbani kwa mkuu wa intelijensia wa Sudan Kusini aliyefutwa kazi hivi karibuni. Haya ni kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukiliita tukio hilo kuwa jaribio la kumkamata.

Majenerali wa jeshi la SPLA
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka wa 2011Picha: picture alliance/AP Photo

Milio ya risasi ilirindima nyumbani kwa mkuu wa intelijensia wa Sudan Kusini aliyefutwa kazi hivi karibuni. Haya ni kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi huku Umoja wa Mataifa ukiliita tukio hilo kuwa jaribio la kumkamata.

Akol Koor alikuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu alipotimuliwa mwezi Oktoba, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini humo, lakini aliendelea kuwa mtu mwenye nguvu. Aliiongoza idara ya usalama wa taifa tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka wa 2011. Mwandishi mmoja wa AFP amesema mapigano hayo kwenye mji mkuu wa Juba yalidumu kwa karibu saa moja.

Soma pia: UN yatoa wito kwa viongozi wa S. Kusini kuhusu uchaguzi

Chanzo cha kijeshi kinachodaiwa kuhusika katika operesheni hiyo kililiambia gazeti la Sudans Post kuwa Koor alikamatwa baada ya mapigano makali yalisababisha askari wake kadhaa kuuawa au kujeruhiwa. Haijabainika wazi kama Koor amekamatwa au la. Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Lul Ruai Koang amesema tukio hilo liliwahusisha wanajeshi wao ambao walitumwa nyumbani kwa Koor kutoa ulinzi wa ziada. Amesema haijafahamika kilichotokea na kuwa hali hiyo ya kutoelewana ilisababisha ufyatulianaji wa risasi.