1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Idadi ya waliopoteza maisha yafikia watu 30

Lubega Emmanuel20 Novemba 2020

Idadi ya waliopoteza maisha yao kufuatia machafuko ya kampeni nchini Uganda imefikia watu 30. Hii ni kwa mujibu wa taarifa za polisi nchini humo.

Afrika | Kenia Uganda Proteste  Bobi Wine Opposition
Picha: AP Photo/picture alliance

Akizungumzia machafuko hayo kwa mara ya kwanza, rais Yoweri Museveni ameonya kuwa wale waliohusika katika kuchochea ghasia hizo watakiona cha mtema kuni na anawalaumu wageni kwa kufadhili machafuko hayo.

Kwa upande wao, wanaharakati wa haki za binadamu wanaikosoa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kwa kushindwa kudhibiti vyombo vya usalama ambavyo inadaiwa vimewaua watu wasio na hatia ambao hawakuwa miongoni mwa waandamanaji. 

Huku taarifa za ghasia za kampeni zikiendelea kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa siku ya tatu mfululizo, polisi imearifu kuwa idadi ya waliopoteza maisha yao imefikia watu 30 na wengine wengi miongoni mwa zaidi ya sitini waliopata majeraha wamo katika hali mahututi.

Bobi Wine baada ya kukamatwa na polisiPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Miongoni mwao ni waandishi habari watatu. Kulingana na taarifa hizo watu 48 wana majeraha ya risasi. Wanaharakati wa haki za binadamu wameshtumu vyombo vya usalama kwa mauaji hayo. Sarah Birete mkurugenzi wa Kituo cha utawala wa kikatiba CCG ni mmojawapo wa wanaharakati aliyekemea machafuko hayo.

Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, mgombea urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alikuwa anatarajiwa kufika mbele ya hakimu mjini Iganga kilomita 110 kutoka Kampala, eneo ambako alikamatwa siku ya  Jumatatu kwa madai ya kukiuka kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19  pale alipowakusanya watu zaidi ya mia mbili. Kucheleweshwa kufikishwa
mahakamani kwa mgombea huyo kumekosolewa na mawakili wake.