Uganda iliingiza silaha Sudan Kusini
29 Novemba 2018Ripoti iliyotolewa leo ya Taasisi ya Utafiti wa Kuzuia silaha katika maeneo ya Migogoro yenye makao yake jijini London, inazusha maswali kuhusu msaada wa Uganda kwa serikali ya jirani yake Sudan Kusini hata wakati ikijinadi kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote katika mgogoro huo ambao ni mojawapo ya vita vikali zaidi barani Afrika.
Mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo James Bevan amesema ripoti hiyo mpya ni picha ya uchunguzi wa kina wa jinsi udhibiti wa uuzaji wa silaha kwa makundi yanayozozana ulivyoshindwa.
Ripoti hiyo inasema Uganda ilinunua silaha kutoka kwa nchi tatu wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo ni Bulgaria, Romania na Slovakia ambazo zilipelekwa kwa jeshi la Sudan Kusini na washirika wao wapiganaji nchini Sudan.
Uhamisho huo ulifanyika kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka marufuku yake ya silaha nchini Sudan Kusini mapema mwaka huu lakini baada ya marufuku iliyotangazwa na Umoja wa Ulaya.
Mike Lewis, mkuu wa operesheni za kikanda katika Taasisi hiyo ya Conflict Armament Research anasema kuhusu silaha za Bulgaria, Sudan Kusini iliitumia Uganda kutoa vyeti vya kutumiwa katika ununuzi wa kimataifa wa silaha ili kufanya ionekane kana kwamba silaha hizo zilikuwa za matumizi ya jeshi la Uganda ilhali ukweli ni kwamba zilipaswa kwenda Sudan Kusini.
Haifahamiki wazi kama serikali ya Uganda, mshirika mkubwa wa Marekani katika usalama wa kanda hiyo, ilishiriki katika uhamishwaji wa silaha ilizopokea kutoka Romania na Slovakia mwaka wa 2015.
Lewis amesema serikali ya Uganda haikujibu ushahidi iliotumiwa na kuwa msemaji wa jeshi Brigedia Richard Karemire aliliambia shirika la AP kuwa hajaiona ripoti hiyo akiongeza kuwa wao wanaunga mkono mchakato wa Amani Sudan Kusini.
Waziri wa habari wa Sudan Kusini Michael Makuei Lueth aliupinga uchunguzi huo kuwa bandia akiliambia shirika la AP kuwa hata hawana fedha za kununua silaha na kwa sasa wanahitaji fedha za kuyafanikisha makubaliano ya Amani.
Makuei aliuliza ni vipi Umoja wa Ulaya ulitangaza marufuku ya silaha na kutarajia wengine kuiheshimu? Anasema kama Umoja wa Ulaya uliweka marufuku ya silaha ni juu yao, maana nchi za Kiafrika sio mwanachama wao na hawafai kutekeleza masharti yao.
Ripoti hiyo inasema, kwa nchi zinazouza silaha, hakuna kitu kinachoashiria kwamba walishiriki katika ukiukaji huo, au hata kufahamu kuhusu kuhamishwa silaha hizo.
Uganda katika siku za nyuma ilitoa wazi msaada kwa serikali ya Sudan Kusini wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe,ambavyo vilianza mwishoni mwa mwaka wa 2013 kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na aliyekuwa wakati huo makamu wake Riek Machar.
Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga