Uganda: Jeshi lasema watu 30 waliuawa na 2,000 wakakamatwa
23 Januari 2026
Kauli ya kutisha ya mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba kwamba wafuasi 30 wa upinzani wameuawa, kauli ya kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine kwamba yuko mafichoni kwa kuhofia maisha yake, na tahadhari ya umoja wa mataifa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Uganda, vimezidisha wasiwasi mkubwa nchini humo baada ya uchaguzi wa rais na bunge wa Januari 15.
Jeshi la Uganda, kupitia mkuu wake Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa rais Yoweri Kaguta Museveni, limedai kuwa wafuasi 30 wa upinzani waliuawa na zaidi ya watu 2,000 kukamatwa baada ya uchaguzi wa Januari 15. Kauli hiyo ilizua ghadhabu kubwa ndani na nje ya nchi, huku mashirika ya kimataifa yakieleza hofu juu ya haki za binadamu kuzidi kuharibika.
Kiongozi wa upinzani Robet Kyagulanyi ali-maarufu Bobi Wine,alisema yuko mafichoni baada ya kudai kuwa wanajeshi walivamia nyumba yake. Alitaja uchaguzi huo kuwa ni "wizi wa wazi” na akasema usalama wake pamoja na wa familia yake uko hatarini.
Bobi Wine aliiambia DW kuwa alilazimika kujificha kwa sababu hakuweza kupata ulinzi kutoka taasisi za serikali, akidai familia yake iko chini ya kifungo cha nyumbani na imezungukwa na wanajeshi, huku chakula kikizuiwa kuingia. "Nchini Uganda, katika nchi ambayo hakuna utawala wa sheria, katika nchi ambayo jenerali wa jeshi anaweza kunywa na kulewa kisha kutamani mtu afe, au akaamuru mtu auawe, na hilo likatokea, katika nchi ambayo jenerali wa jeshi ambaye pia ni mtoto wa rais wa nchi hiyo, na kama unavyojua anawatesa watu hadharani mbele ya kamera, hakuna usalama. Hakuna mtu aliye salama. Tunafanya nini? Je, tunajisalimisha na kuchinjwa? Hapana. Hatufanyi hivyo. Tunapambana."
Kiongozi huyo wa chama cha NUP chenye ufuasi mwingi miongoni mwa vijana pia alisema hana imani na mahakama za Uganda, akizituhumu kufanya kazi kwa niaba ya utawala uliopo, na kuwataka raia wa Uganda kuendelea kupinga unyanyasaji kwa njia zisizo za vurugu, ikiwemo maandamano na uasi wa kiraia.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali hiyo. Katibu Mkuu wa umoja Antonio Guterres alisema anafuatilia kwa karibu matukio ya baada ya uchaguzi, hasa ripoti za kukamatwa kwa wapinzani na kuzuiliwa na vurugu dhidi yao. "Katibu Mkuu anafuatilia kwa wasiwasi hali ya baada ya uchaguzi nchini Uganda, ikiwemo taarifa za kukamatwa, kuzuiliwa na matukio ya vurugu yanayohusisha viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Anasisitiza umuhimu wa kujizuia kwa wahusika wote na kuheshimu utawala wa sheria pamoja na wajibu wa Uganda chini ya mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu ikiwemo haki ya uhuru wa kujieleza, kushirikiana na mikusanyiko ya amani. Katibu Mkuu anasisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria na kuwaheshimu na kuwatendea haki watu wote walioko mahabusu, akibainisha umuhimu wa kulinda nafasi ya kiraia."
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wametoa wito kwa pande zote kujizuia, kuheshimu utawala wa sheria na kulinda haki za msingi za binadamu, huku wakionya kuwa hali ya sasa inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi hiyo ikiwa haitashughulikiwa kwa haraka.