Uganda Kupambana na Ugonjwa wa Fistula
3 Desemba 2013Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya nchini Uganda mwaka huu, takwimu zinaonyesha, asilimia 2 ya wanawake waliofika umri wa kuzaa wameshaugua ugonjwa wa fistula, sawa na idadi ya wanawake takriban140,000 hadi 200,000, ingawaje idadi kamili haijajulikana, kutokana na unyanyapaa uliokithiri dhidi ya waathirika wa ugonjwa huo na kufanya wengi wao kuona haya kujitokeza kupata matibabu.
Unyanyapaa wa wagonjwa wa fistula
Kutokana na tatizo la wagonjwa wengi wa Fistula kutojitokeza, Dr Susan Obare, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa aina hiyo katika hospital ya Taifa Mulago nchini Uganda, anasema idadi kamili haifamiki na hali hiyo ya kutojitokeza wanawake wanaougua maradhi hayo, imetokana zaidi na unyanyapaa wanaokabiliana nao. Mary ni mwanamama anayefanya shughuli za ukulima, katika wilaya ya Mubende na amekuwa akiugua maradhi hayo, tangu alipojifunguwa mtoto ambaye alikuwa hajatimia wakati wa kuzaliwa miaka 15 iliyopita. Mary mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akitokwa na mikojo kila wakati hali ambayo ilimfanya kushindwa hata kwenda sokoni au kanisani.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa kitabibu, bibi huyo anaugua kile kinachojulikana kama Obstetric Fistula, maradhi ambayo yanatokana na kuwepo kwa tundu kati ya uke na kibofu cha mkojo au sehemu ya uke na utumbo, hali ambayo inasababisha mkojo au choo kutoka ovyo kupitia uke. Kismingi matatizo hayo zaidi yanasababishwa na mtu kupata maumivu au uchungu wa uzazi wa kwa muda mrefu wa zaidi ya saa 24 wakati wa kujifunguwa.
Kwa mwanamama Mary, binafsi alipata uchungu wa uzazi kwa muda wa siku tatu na kwa kuwa hospitali ilikuwa mbali na mahala anapoishi, alipelekwa katika zahanati ndogo tu ambako alikaa kwa saa 48 akijaribu kujifunguwa mwanawe.
Huduma duni za uzazi kuleta madhara
Siku ya tatu ndipo alipopelekwa katika hospitali ya wilaya, ambako alifanikiwa kujifunguwa mtoto huyo aliyekuwa ahajatimia muda. Akisimulia madhila yaliyompata kutokana na kuuguwa ugonjwa huo wa Fistula, mwanamke huyo anasema alitelekezwa na mtu aliyempa ujauzito na baadae hata familia yake mwenyewe ilimtenga.
Hata hivyo licha ya wanawake wengi nchini Uganda kujikuta wakiuguwa maradhi hayo, nchi hiyo inakabiliwa pia na tatizo la kuwa na idadi ndogo ya madaktari wa upasuaji waliopata mafunzo yanayohitajika katika kuwafanyia upasuaji wagonjwa hao. Kwahivi sasa kuna madaktari 24 pekee katikaa nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye idadi ya watu kiasi milioni 34 hadi 37.
Kutokomeza Fistula Uganda
Mtaalamu wa kitaifa wa maradhi hayo Peter Mukasa anasema wanawake 1900 wanapata maradhi hayo kila mwaka na wanaoweza kufanyiwa upasuaji kila mwaka ni wanawake 2,000, kutokana na changamoto hiyo Daktari Mukasa anahisi itachukuwa miaka mingi kwa Uganda kuweza kulimaliza tatizo hilo. Tatizo lakini sio tu la ukosefu wa madaktari bingwa katika kuutokomeza ugonjwa huo, bali hata gharama ya matibabu yake iko juu kiasi cha wengi kushindwa kuimudu. Daktari Mukasa anasema, matibabu ya upasuaji wa kuponya Fistula yanafikia kiasi cha dolla 400 ikiwemo gharama ya usafiri wa kwenda hospitali kulazwa na huduma nyingine.
Pamoja na hayo lakini amefahamisha kwamba, kiasi kikubwa cha gharama hizo kinasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya idadi ya watu UNFPA. Ingawa kwa upande mwingine daktari Susan Obore, anasema yapo matumaini nchini Uganda ya kuutokomeza kabisa ugonjwa huo na hilo litawezekana kupitia kuwapa uwezo zaidi wanawake katika kuzuia Fistula.
Mwandishi: Diana Kago/IPS
Mhariri: Mohammed AbdulRahman